November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi aumwagia sifa uongozi wa Samia

Na Penina MalundoTimesmajiraonline,Dar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema wakati huu wa kuadhimisha miaka 60 ya Muungano, wanaridhishwa na utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo umempatia sifa nje ya nchi na amewezesha kuwezesha nchi kupiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta zote ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake.

Pia, amepongeza Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika uandaaji wa makongamano mbalimbali ambayo yanaleta tija kwa jamii ya Watanzania.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipofungua mdahalo wa kitaifa wa wanawake na Muungano uliondaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

“Bila ya shaka utendaji na mchango wa viongozi hawa umefanya wanawake wenzao kuendelea kuaminika katika nafasi mbalimbali za uongozi kama anavyodhihirisha hilo Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hakika sote tunaridhika na utendaji wake ambao umeipatia sifa nchi yetu na kutuwezesha kupiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta zote katika kipindi kifupi cha uongozi wake.”

“Tunamwomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema, hekima na uwezo wa kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa mafanikio na viongozi wote wanawake wanaowatumikia Watanzania katika nafasi mbalimbali za uongozi,” amesema.

Amesema katika kuenzi Muungano ameahidi viongozi wa pande zote mbili wataendelea kuchukua hatua za kujadiliana na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano zilizobaki.

“Historia inawataja wanawake mbalimbali walioshiriki kwa hali na mali katika harakati za kupigania uhuru wa iliyokuwa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,”anasema.

Rais Mwinyi alieleza wanawake hao na wengine walioshika nafasi mbalimbali za uongozi nchini na vyama vya siasa na jumuiya zake wanabaki kuwa ni vigezo vizuri vya utendaji na ushiriki wa wanawake katika kuleta maendeleo ya Watanzania.

Rais Mwinyi amesema Muungano ambao unatimiza miaka 60 leo ya kuasisiwa kwake umeiletea sifa za kipekee na heshima nchi na faida nyingi za kikuchumi, kisiasa na kijamii kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

“Dhamira njema ya waasisi wa Taifa letu ya kuunganisha nchi zetu mbili imeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili za muungano kwa kuudumisha na kuimarisha kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza hadi sasa, hivyo kuufanya uwe imara zaidi,” amesema