Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,ameongoza maelfu ya Wazanzibar kushiriki siku ya kitaifa ya mazoezi Zanzibar kwenye uwanja wa Mnazi mmoja wilayani Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambayo ni sehemu tu ya shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12,2025.
Dkt.Mwinyi,aliongoza mazoezi hayo Januari Mosi,2025,ambapo ameipongeza benki ya NMB, kuendelea kuunga mkono shughuli mbalimbali za Serikali yake, ikiwemo shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar,ambayo imedhamini na kushiriki siku ya kitaifa ya mazoezi na michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Ambapo benki hiyo ilikabidhi ‘tracksuit’ 100 za kuvaa viongozi, zikiwa na thamani ya milioni 9, huku ikidhamini michuano ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup 2025) kwa milioni 50, mchango uliomsukuma Rais Mwinyi kuiomba taasisi hiyo kudumisha ushirikiano huo.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inatambua, inathamini na kujali mchango wenu kwa maendeleo na ustawi wa Wazanzibar. SMZ inaamini mtaendelea kushirikiana nayo katika kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa,” amesema Dkt. Mwinyi.
Naye Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Naima Said Shaame,amesema benki hiyo imekuwa mshirika wa shughuli mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
“Ni mwaka wa 12 sasa NMB inashirikiana na SMZ kufanikisha sherehe za Mapinduzi, ambako mwaka huu tumekabidhi ‘tracksuit’ za mazoezi 100 zenye thamani ya milioni 9, tukiamini kwamba mchango huo utakuwa chachu ya kuhamasisha mazoezi visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wake,”.
“Pia, tumetoa milioni 50 kudhamini Kombe la Mapinduzi, udhamini ambao pamoja na ‘tracksuit’ hizo, tunaamini kwamba, ni kielelezo na uthibitisho wa dhati kuwa NMB inathamini michezo, kwani afya zetu zinaimarika zaidi kupitia michezo na uimara wa afya ndio chachu ya kukua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,”.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili