October 3, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi afanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na Naibu Mawaziri, huku ACT-Wazalendo ikipata nafasi nne za uwaziri katika hatua inayolenga kukamilisha uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Dkt. Mwinyi ametangaza mabadiliko hayo leo, Oktoba 3, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu Zanzibar.

Katika uteuzi huo, viongozi wanne kutoka ACT-Wazalendo wamepewa nafasi za uwaziri.

Nassor Ahmed Mazrui ameteuliwa kuwa Waziri wa Afya, wakati Omar Said Shaaban ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda.

Aidha, Dkt. Nasra Nassor Omar ameteuliwa kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, huku Dkt. Mohamed Ali Suleiman akiteuliwa kuwa Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu.

Mabadiliko ya miundo ya Wizara

Mbali na uteuzi huo, Rais Mwinyi ametangaza mabadiliko katika muundo wa baadhi ya Wizara na taasisi za Serikali.

Miongoni mwa mabadiliko hayo ni kuhamishiwa kwa masuala ya mipango katika Ofisi ya Rais, Ikulu, pamoja na kuanzishwa kwa Wizara mpya ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Katika mabadiliko hayo, Shaaban Ali Othman ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Mipango na Usimamizi wa Utendaji Serikalini.

Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu, anayeshughulikia Uhusiano wa Jamii.

Wengine walioteuliwa ni Mudrik Ramadhan Soraga, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, pamoja na Ali Suleiman Ameir Mrembo, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Naibu Mawaziri nao wafanyiwa mabadiliko

Rais Mwinyi pia ametangaza mabadiliko katika nafasi za Naibu Mawaziri katika Wizara mbalimbali.

Mabadiliko hayo yamehusisha Wizara za Afya, Kilimo, Elimu, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Fedha, Utalii na Mambo ya Kale, pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji.

Kwa mujibu wa Rais Mwinyi, mabadiliko hayo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya maridhiano yaliyofikiwa baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Uapisho Oktoba 5

Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa pamoja na wale waliohamishwa katika nafasi mbalimbali wanatarajiwa kuapishwa Jumatatu, Oktoba 5, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hafla ya uapisho itafanyika saa 8:00 mchana.