Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZIRI wa Nishati, Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi pamoja na wanachama wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (TAOMAC), kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mafuta, pamoja na kujadili namna ya kuboresha na kukuza sekta hiyo nchini.
Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, ambapo Dkt. Homera amepata fursa ya kufahamiana na wanachama wa TAOMAC na kusikiliza maoni pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji na maendeleo ya sekta ya mafuta nchini.
Katika kikao hicho, pande hizo zimejadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha usimamizi na ufanisi wa sekta ya mafuta, ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha na kwa wakati katika maeneo yote ya nchi, kwa ajili ya kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Homera amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya mafuta katika kuhakikisha usalama wa upatikanaji wa mafuta nchini, akieleza kuwa mafuta ni nishati muhimu inayotegemewa kwa kiasi kikubwa katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya Serikali, waagizaji na wasambazaji wa mafuta katika kutambua na kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza, ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa na ufanisi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Mafuta, Goodluck Shirima; viongozi wa Menejimenti za Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), pamoja na viongozi na wanachama wa TAOMAC.


More Stories
Ndejembi apeleka ujumbe wa Tanzania Afrika
Rais Mwinyi afanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
Kamati ya Bunge: Chakula kipo cha kutosha nchini