Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli lamekagua maandalizi ya kumbi za mikutano na vikao vya chama vinavyotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Rais Magufuli akiwa ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Bashiru Ally Kakurwa amekagua kumbi za Kituo cha Mikutano Dodoma (Jakaya Kikwete Hall) ambako utafanyika Mkutano Mkuu wa CCM na pia amekagua jengo la Ofisi za Makao Makuu ya CCM (White House jijini Dodoma).
Pia Rais Magufuli amewapongeza wajumbe wa Sekretarieti ya CCM na wasimamizi wa ukarabati uliofanyika katika majengo hayo ya CCM ambayo yanatarajiwa kuwa tayari ifikapo tarehe 20 Juni, 2020.

Magufuli amesisitiza kuwa, pamoja na kufanyika kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama, Uchaguzi Mkuu lazima utakuwepo na hivyo amewataka wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha kugombea nafasi wanazoomba.
Ameonya kuwa kuelekea katika mchakato huo wanachama hawana budi kuweka mbele maslahi ya chama badala ya maslahi yao binafsi na pia kutofanya vitendo vya kuwagombanisha na fujo ambavyo vitakavyokiumiza chama.
“Chama chetu kinayo demokrasia ya kutosha, lakini demokrasia hii ndani ya chama isije ikatumika kuleta fujo, kutugombanisha na kukiumiza chama, tuweke maslahi ya chama mbele na tutumie nafasi hii kukiimarisha chama chetu,” amesema Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli amewataka wana CCM kote nchini kutembea kifua mbele na kuyasema mambo yote ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wananchi, badala ya kuacha jukumu hilo kwa viongozi wachache.
More Stories
Serikali ,Washirika wa Maendeleo waweka mkakati utekelezaji Dira ya 2050
Benki ya Exim yazindua suluhisho la malipo ya kisasa kwenye Z- Summit 2025
DCEA yateketeza zaidi ya ekari 300 za bangi