December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Magufuli aitakia heri Taifa Stars, aahidi neema kwa wasanii

Na Shamimu Nyaki- WHUSM, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli ameitakia heri timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika mechi ya leo dhidi ya timu ya taifa ya Tunisia pamoja na Bondia Hassan Mwakinyo katika pambano la kuwania ubingwa wa WBF dhidi ya Bondia Carlos Paz wa Argentina.

Taifa Stars’ leo usiku itakuwa katika uwanja wa Stade Olmpique de Rades kusaka ushindi mbele ya wenyeji wao Tunisia katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2021).

Dkt.Magufuli ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akihutubia na kufungua Bunge la 12, ambapo ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itatenga fedha kidogokidogo kwa ajili ya kuziandaa timu za taifa katika mashindano mbalimbali.

“Nitumie fursa hii kuitakia kila la heri timu yetu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Tunisia, namtakia heri pia Mwanamasubwi wetu Hassan Mwakinyo katika pambano lake baadaye leo. Watanzania tunakata ushindi, tumechoka kushindwashidwa” amesema Rais Dkt. Magufuli.

Katika hotuba hiyo, Dkt. Magufuli ameeeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya Sanaa, Utamaduni pamoja na Michezo ambazo zinakua kwa kasi hivi sasa huku akiahidi kuhuisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ili kuwasaidia wasanii kupata mafunzo ya sanaa pamoja na mikopo.

Aidha Dkt.Magufuli amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo Serikali itaimarisha usimamizi wa Hakimiliki za wasanii ili wanufaike na kazi zao pamoja na kuchangia pato la Taifa.

“Tutahakikisha tunaimarisha zaidi sekta ya michezo hasa usimamizi wa masuala ya hati miliki ili wasanii waweze kunufaika na kazi zao, ninafarijika kuona kuna wasanii ambao ni wabunge miongoni mwetu humu. Tutauwisha pia mfuko wa utamaduni wa sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu ikiwemo kupata mafunzo na mkopo,”.

“Lakini pia tutaanza kutenga pesa kidogo kidogo kwa ajili ya kuziandaa timu zetu za
Taifa na katika hilo napenda kutumia fursa hii kuitakia kheri timu yetu ya taifa ya ‘Taifa Stars’ kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia baadae leo pamoja na wanamasumbwi wetu, Hassan Mwakinyo ambaye anapambano leo. Watanzania tunataka ushindi, tumechoka kushindwa shindwa,” amesema Magufuli.