May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia aongoza mazishi ya Lowassa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Monduli

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza viongozi mbalimbali wa Kiserikali na vyama vya kisiasa katika ibada ya mwisho ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Edward Ngoyai Lowassa katika Kijiji cha Ngarash.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo Februali 17, Mwaka huu katika ibada ya mwisho iliyofanyika nyumbani kwa Hayati Lowassa, akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali akiwemo, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine.

Rais Samia, amesema yapo mengi aliyojifunza kwa Hayati Lowassa, ikiwa pamoja na ushupavu, ustahimilivu na ulezi, huku akiwataka watanzania kumuenzi kwa kutenda yaliyo mema.

Amesema, Taifa limepoteza kiongozi na aliyekuwa mwana Mapinduzi wa kweli katika upande wa maendeleo na asiyependa kutumbishwa katika maamuzi yake, hali iliyofanya kuacha historia kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.

” Tumepoteza kiongozi mahiri, mwana Mapinduzi wa kweli na aliyekuwa na upendo kwa kila mmoja, hivyo ni vyema kumuenzi kwa kuyaishi yale yaliyo mema. Kuna mambo matatu nimejifunza kutoka kwake na ambayo pia ninaona ni ya muhimu, mambo hayo ni pamoja na ushupavu, ustahimilivu na ulezi hivyo ni vyema kila mmoja akayaishi haya”, amesema Rais Dkt.Samia.

Pia amesema kuwa, Lowassa katika maisha yake ya utumishi na uongozi wa umma, alikuwa mfano mzuri wa kiongozi na mlezi kwa vijana kutoka nyanja mbalimbali, huku akitolea mfano wa kipindi cha maisha yake ya siasa na hata mwaka 2015 akigombea nafasi ya Urais moja ya kipaumbele chake ilikuwa ni elimu.

” Mbali na hayo, pia Lowassa alikuwa mfano mzuri wa kiongozi na mlezi mzuri kwa vijana na hata mwaka 2015 wakati akigombea Urais moja ya kipaumbele chake ilikuwa ni elimu elimu elimu na ndiyo maana aliweza kuanzisha hata shule za Kata na sisi kama Serikali tunaendelea kuziboresha”, ameongeza Rais Dkt. Samia.

Aidha aliongeza kuwa, Lowassa alikuwa ni kiongozi ambaye katika kipindi chote cha uongozi wake, hususani upande wa siasa hakupenda kuvisema vibaya Vyama vingine kwa lugha za matusi wala kulumbana na badala yake alitumia hoja zenye mashiko hadi kupelekea kuelewana.

“Ndugu zangu, ni vyema tukaishi katika Yale aliyoyaishi ndugu yetu Lowassa hususani katika upande wa siasa, yeye alikuwa si mtu wa kutumia lugha za kejeri na malumbano na badala yake alitumia hoja zenye mashiko na mkaelewana..tukistahimili Taifa litabaki salama kwa kufanya siasa za kistaarabu”, ameongeza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema namna nzuri ya kumuenzi Lowassa ni kutenda mema na kumuombea, huku akiishukuru Kamati ya kitaifa kwa kazi nzuri waliyofanya kwa kipindi chote cha maombolezo.

Nae Mtoto wa Hayati Lowassa, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Fredrick Lowassa amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa upendo alioonesha katika familia hiyo wa kujitokeza pesa ya mfukoni mwake kwa familia hiyo, ili kuweza kumuwaisha Hayati Lowassa Afrika ya Kusini kwa ajili ya matibabu wakati akiwa amezidiwa, kwani bado taratibu za kiserikali zilikuwa zinaendelea kufanyika ili apelekwe.