Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iandae mpango mkakati wa kurekebisha makambi ya vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili malezi ya vijana hao yatekelezeke kwa ukamilifu na kuleta tija inayotarajiwa kwa Taifa.
Rais Samia ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JKT tangu kuanzishwa kwake Julai 10,1963.
“Nimeelezwa hapa kuwa JKT inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchache na uwezo mdogo wa makambi kuchukua vijana ,upungufu wa zana mbalimbali uchakavu wa miundombinu wa makambi na muda mdogo wa mafunzo kwa vijana wa mujibu wa sheria unaosababisha mafunzo kutotolewa kwa ukamilifu.”amesema Rais Samia
Aidha Rais Samia amelitaka Shirika la Uzalishaji Mali la JKT SUMAJKT, liingie kwenye mikopo itakayoliwezesha Shirika hilo kusonga mbele katika uzalishaji na kuongeza tija katika pato la Taifa
“Kwa hiyo kama kutatakiwa udhamini wa serikali au vyovyote serikali tupo tayari kuwezesha SUMAJKT ili iweze kuzalisha kwa kiwango kikubwa.”
Amesema,dhamira ya serikali ni kuliboresha JKT ili liwe jeshi la kisasa zaidi linaloendana na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu huku akisema,Mafunzo yanayotolewa na JKT yawasaidie vijana kuwa wazalendo wa kweli wanaothamini utaifa, umoja na mshikamano wa watanzania na wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea.
Katika hatua nyingine amelipongeza Jeshi hilo kwa mafanikio lukuki yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ikwemo malezi ya vijana ambayo yamechangia kuimarisha umoja hapa nchini.
Kwa mujibu wa Rais Samia mbali na kupewa mafunzo yote hayo ya msingi JKT limekuwa likitoa mafunzo na ujuzi mbalimbali kwa vijana ikiwa ni pamoja na kazi za mikono kitendo kinachowafungua vijana hususan waliosoma taaluma mbalimbali na kudhani kwamba taaluma walizosomea haziwaruhusu kufanya kazi za ujuzi mwingine ikiwemo kazi za mikono,na hivyo vijana kuweza kujitegemea
“Yote haya yanayofanywa ndani ya Jeshi hili ni kutekeleza dira ya nchi yetu ambapo kwa sasa tunatekeleza dira ya 2025 ambayo kwa msisitizo mkubwa imeelekeza kujenga uzalendo utaifa na kuimarisha umoja ,
“Lakini tukiacha dira JKT linakwenda kutekeleza mpango wa tatu wa miaka mitano unaotekelezwa nchini kwetu unaotarajiwa kumalizika 2026/27 na mpango huu na wenyewe umehimiza mambo kadhaa lakini jambo kubwa ni kuchagiza wajibu wetu wa kutumia rasilimali za ndani ili kuondoa utegemezi bila kusahau mila na desturi zetu.”ameongeza kuwa
“Aidha mpango umehimiza kuendeleza na kuimarisha vyuo vya ufundi na ufundi stadi na hili nalo linafanywa kwa kiasi kikubwa na JKT ..,pia mpango wa miaka mitano umehimiza uwezeshaji wa vijana ,na katika uwezeshaji wa vijana kuna matawi kadhaa ikiwa ni pamoja kuwawezesha vijana kufunguka kiuchumi na kuwa na fikra nzuri na nchi yao lakini pia JKT linatengeneza ajira jambo ambalo limesisitizwa kwenye mpango wa miaka mitano.”
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema,JKT inajukumu kuu la malezi kwa vijana lakini pia inapaswa pia kuwa na ubunifu na kutoa mchango katika Taifa hasa katika uzalishaji wa ajira kwa vijana na kusaidia taifa kuwa na uhakikika wa chakula .
Naye Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda amesema kuwa Jeshi la kujenga Taifa linatekeleza shughuli za uzalishaji Mali Kwa Taifa huku likiendelea na majukumu yake ya msingi ya malezi ya vijana.
“Jeshi la kujenga Taifa limefankkiwa Kwa kiasi kikubwa kutimiza malengo hayo kwani vijana wetu waliopatiwa mafunzo wamekuwa mfano mzuri na wakuigwa katika jamii yetu,maeneo ya kazi na Uongozi na hata katika kuendesha maisha yao binafsi,”amesema
Awali Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema kuwa Jeshi la kujenga Taifa limeendelea kupata mafanikio mengi katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya malezi ya vijana, uzalishaji Mali na Ulinzi wa Taifa.
More Stories
Maandamano ya kuunga mkono Samia, Mwinyi yatikisa Tabora
Haya hapa matokeo yote kabisa ya Form Four
Kisarawe kukata keki Birthday ya Rais Samia