Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema watendaji wa taasisi za Serikali wanawajibu wa kutekeleza maagizo na maamuzi yanayotolewa na Serikali kuu katika kuleta ufanisi wa kuharakisha maendeleo ya nchi.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipozindua mwongozo wa uwekezaji Zanzibar wa mfumo wa kielektroniki kwa Mamkala ya Uwekezaji Zanzibar, ZIPA katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Wilaya ya Magharibi B.
Rais Dk. Mwinyi alisema lengo la Serikali ya kuzindua mfumo huo ni kuharakisha utoaji wa huduma rahisi kwa wawekezaji ikiwemo kusajili, upatikanaji cheti cha uwekezaji na huduma nyengine zinazotolewa na kituo hicho.
“Ni Matumani yetu, mfumo huu utasaidia kupunguza usumbufu, kuongeza mapato na kupunguza gharama zinazomlazimu mwekezaji” Alisema Dk. Mwinyi.
Alisema, mfumo huo wa kielektroniki utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ZIPA pamoja na kuondosha urasimu usio wa lazima na kasi ya utendaji Serikalini.
Aidha, alisema Serikali inaweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini pamoja na kuchukua hatua stahiki za kuondosha vikwazo vyote vya kisheria na mifumo inayozuia mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
Alisema mfumo huo utarahisisha ufuatiliaji taratibu zote zinazohusika hadi mradi unasajiliwa na muhusika kupatiwa cheti chake cha uwekezaji
Dk. Mwinyi alieleza uwekezaji ni sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi katika kukuza uchumi na kuanzisha fursa za ajira, aliongoza Zanzibar imefungua milango ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini ili kuunga mkono juhudi za serikali.
Alisema Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kwa kuhakikisha mazingira salama ya biashara na uwekezaji unaendelea kuimarika Zanzibar.
“Tunaamini ongezeko la uwekezaji ni muhimu kwa nchi yetu katika kutekeleza mipango ya Maendeleo ya Kitaifa….” Alisema Dk. Mwinyi.
Akizungumzia maendeleo ya miradi ya uwekezaji nchini Dk. Mwinyi alisema kwa kipindi cha miaka miwili Serikali imesajili miradi 226 yenye thamani ya mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 3.5 ambayo inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 13,500.
Kuhusu sekta ya uchumi wa buluu Dk. Mwinyi alieleza sera kuu ya serikali ni kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hiyo na kueleza mikakati ya uchumi wa buluu imejikita kwenye kuweka matumizi mazuri ya rasilimali za bahari na kulinda mazingira ya bahari.
Aidha, alieleza hatua za serikali katika ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani Sekta ya mafuta na gesi, usafiri wa bandari na Miundombinu katika eneo la uchumi wa buluu.
Akizungumza kwenye halfa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, watendaji wa taasisi za Serikali wanawajibu wa kutekeleza maagizo na maamuzi yanayotolewa na Serikali kuu alisema ufunguzi wa mfumo huo utaisaidia Wizara kuitangaza zaidi Zanzibar kimataifa kupitia sekta ya uwekezaji pamoja na kuleta mapinduzi ya utoa wa huduma bora na kuharakisha utendaji kwa taasisi zinazotegemeana kufanikisha uwekezaji nchini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharrif Ali Sharrif alieleza lengo la taasisi hiyo ni kuwa kitovu cha kutoa huduma bora Afrika Mashariki na Kati.
Mwongozo, huo uliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), unaelekeza taratibu zote muhimu za uwekezaji na wawekezaji kwa lengo la kurahisisha na kufanikisha usajili wa miradi ya uwekezaji nchini.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato