December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Mwinyi ahimiza kuhifadhi Qur’aan

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya kiislamu kuendelea kuhifadhi Quran Tukufu na kufundisha watoto wao kuisoma na pia wazidishe kutoa sadaka kwa watu wenye mahitaji hususani katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo katika fainali za 24 za Mashindano ya Quran Tukufu Afrika yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al Hikma Foundation kwa kushirikisha nchi mbalimbali 22 za Afrika na nje ya Afrika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam tarehe 24 Machi 2024.

Aidha Rais Dkt. Mwinyi amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano na kuzidi kupiga hatua za maendeleo nchini.

Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Taasisi ya Al Hikma Foundation kwa kuandaa mashindano hayo makubwa ambayo yanaitangaza Tanzania kwa kushirikisha nchi mbalimbali.

Pia ameipongeza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kuyadhamini mashindano hayo kila mwaka.

Mshindi wa kwanza wa Mashindano hayo ni Ibrahim Sow wa Ivory Coast aliyepata shilingi milioni 27, mshindi wa pili Haafith Abdulkariim Kabiito kutoka Uganda shilingi milioni 17.2 , mshindi wa tatu Kamil Almin Swaleh kutoka Tanzania shilingi milioni 11.6 , mshindi wa nne Kamilou Koura kutoka Togo shilingi milioni 8.1 na mshindi wa tano Idris Nshimwe kutoka Burundi shilingi milioni 4.5