Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Waumini wa Kanisa la Anglikana kufuatia kifo cha Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Augustino Ramadhani kilichotokea leo asubuhi tarehe 28 Aprili, 2020 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli amesema Marehemu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani atakumbukwa kwa utumishi uliotukuka kwa nchi yake, ulioshadidishwa na umahiri wake, ukweli, uchapakazi, uzalendo wakweli, na ucha Mungu.
“Nakumbuka nilipokwenda kumuona hospitali mazungumzo yake yalikuwa ni ya kumtumaini na kumtegemea Mungu, kwa hiyo na mimi namuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempa pole Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na amemuomba kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani, Majaji, Mahakimu na Wafanyakazi wote wa Mahakama pamoja na Waumini wa Kanisa la Anglikana kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Raha ya milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Augustino Ramadhani astarehe kwa amani, Amina.
imetolewa na Kurugenzi ya Habari Ikulu

More Stories
Matukio katika picha wahitimu Chuo cha Ulinzi
Waziri Ndejembi azindua mradi wa njia ya kusafirisha Umeme, Masasi hadi Newala
Serikali yatangaza neema kwa wakulima