December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Railway Children Africa kurejesha watoto 200 kwenye familia zao

Na Judith Ferdinand, TimesMajira,Online Mwanza

WATOTO 200 wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanatarajiwa kurejeshwa nyumbani kwao kuanzia Aprili hadi Desemba, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya jitihada ya kupunguza ongezeko la watoto hao.

Hayo yamesemwa na Meneja Mradi wa Shirika linalojishughulisha kuwasaidia watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani la Railway Children Africa (RCA), Abdallah Issa wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya watoto na vijana walionufaika na shirika hilo kupitia Mradi wa Kivuko unaoendeshwa.

Issa amesema, tangu mwaka 2018 hadi 2020 shirika hilo limefanikiwa kuwarejesha nyumbani watoto 272 waliokuwa wanaishi nakufanyakazi mitaani katika Jiji la Mwanza pamoja na kuwarejesha shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo na kuwapatia mahitaji ya shule wao na wadogo zao.

Amesema kuanzia Aprili hadi Desemba mwaka huu wanatarajiwa kuwarejesha nyumbani watoto 200 wanaoishi na kufanya kazi mtaani, huku watoto wengi wakitoka Ngara, Bukoba,Ukerewe,Tarime na Sengerema.

Amesema shirika hilo linafanya kazi katika mikoa saba nchini lengo likiwa ni kuwasaidia na kuhakikisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani wanawarudishwa nyumbani, kwani wanaamini kila mtoto ana nyumbani kwao.

Kwa upande wa vijana. amesema wanajitahidi kuwapatia mafunzo ya kujitambua, mitaji ya biashara na kuwapeleka katika vyuo ili kusomea fani mbalimbali ambazo zitasaidia wao kupata ujuzi wa kuweza kujiendeleza na kuendesha maisha yao.

Emmanuel John (wa kwanza kushoto) ambaye ni miongoni mwa vijana waliokuwa wakiishi na kufanyakazi mtaani Jijini Mwanza, akiendelea kutengeneza gari ikiwa ni sehemu mafunzo kwa vitendo katika gereji iliyopo Igogo,baada kuwezeshwa na Shirika la Railway Children Africa kujifunza fani ya ufundi magari kwa lengi la kuwawezesha kupata ufuzi utakaowasaidia kufikia ndoto yao. picha na Judith Ferdinand.

“Mwanza tuna mradi wa miaka mitatu ambao umeanza Aprili 2018 na unaisha Machi mwaka huu, umefanya kazi na vijana, watoto na familia zao, ambapo kwa kipindi chote tumeweza kuwasaidia watoto na kuwarejesha nyumbani 272, kutoka kwenye mikoa mbalimbali na tumewarejesha shule pamoja na wadogo zao.

Tumewasaidia huduma ya afya watoto 537 ambao tumekutana nao mitaani na waliowarejesha nyumbani, vijana 221 tumewapatia mitaji wanaoishi na kufanya kazi mtaani,miongoni mwao wamepelekwa katika kusomea fani mbalimbali ikiwemo udereva na ufundi magari,” amesema Issa.

Pia amesema wanafanya kazi kwa ukaribu na Serikali kwa kushirikiana na TAMISEMi, Wizara ya Afya, Serikali ya Mkoa wa Mwanza kwa Wilaya za Ilemela na Nyamagana na maeneo yote ambayo wamerudisha watoto, ambapo kwa kushirikiana na UNICEF wameweza kuwapa mafunzo maofisa ustawi 60 kutoka Wilaya hizo.

Amesema maofisa hao wanawafundisha watu wa kuaminika namna ya kuwalea watoto hao kabla ya kurejeshwa nyumbani.

Mmoja wa watoto waliofanikiwa kurejeshwa nyumbani na kupelekwa shule kuendelea na masomo na Railway Children Africa, Athumani Juma (siyo jina halisi) alisema kilichopelekea akatoroka nyumbani ni baada ya baba take kufariki na mama yake kutokuwa na uwezo wa kuendesha maisha.

Amesema alizunguka sana mitaani na ametembea maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mwanza, Kahama, Shinyanga, Arusha, Moshi, Mbeya na Dar-es-Salaam,lengo likiwa ni kutafuta unafuu wa kuweza kusaidia familia yake.

Hata hivyo amesema alipokuwa akipata fedha wakubwa walikuwa wanamnyanganya, hali inayofanya kufikiria kurudi nyumbani ingawa kurudi unaogopa.

“Niliamua kukimbilia Dar-es-Salaam kwenye kituo cha Child In The Sun, ambapo walinianzisha darasa la nne na walinishauri nisikate tamaa baada ya mwaka kuna mtu wa shirika la Railway Children Africa alituuliza nani anataka kurudi kwao.

Mimi nikawa miongoni mwa waliojitokeza na baada ya jitihada za kuipata familia yangu nilirudishwa nyumbani pamoja na kupelekwa shule ambapo kwa sasa nipo darasa la tano,” na kuongeza;

Meneja Mradi wa Shirika linalojishughulisha na kuwasaidia watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani la Railway Children Africa (RCA), Abdallah Issa akizungumza na waandishi wa habari (hapo pichani) jijini Mwanza.

“Nalishukuru shirika la Railway Children Africa kwa sasa nakaa na familia yangu na shule nimerudi vizuri nimejitambua, shuleni nafanya vizuri,wamenipatia sare na mahitaji ya shule pamoja na chakula ninachokula ni wao nataka nisome ili nije kusaidia familia yangu na jamii inayonizunguka.

Ndoto yangu nikimaliza masomo nije kuwa mhandisi wa magari,watoto wenzangu wasikate warudi nyumbani na wasome mjini hakuna dili.”

Naye mmoja wa vijana ambaye alikuwa anaishi mtaani lakini sasa ni mmoja wa wanufaika wa shirika la Railway Children Africa ambaye anasomea fani ya ufundi wa magari, Emmanuel John, alisema baada ya kukutana na shirika hilo alipatiwa mafunzo ambayo yamemsaidia kujitambua pamoja na kuwezeshwa kujifunza fani ya ufundi wa magari upande wa injini.

“Nilivyoingia mtaani nilikuwa vizuri, lakini nikabadilika nikawa ninashinda njaa lakini nilikutana na vijana wengine nikaanza kuvuta bangi nikaanza kuwa na tabia mbaya natukana na kufanya vitu vya ajabu ambavyo nikikumbuka naona aibu,lakini baada ya kukutana na Railway Children Africa nimebadilika situkani, nilishukuru sana shirika hili kwa sasa nikimaliza ufundi huu natarajia kuwa fundi mkubwa na kuelimisha wengi, pia vijana wenzangu waachane na tabia mbaya badala yake wajitambue,”alisema John.