Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limefanikiwa kumkamata mwanaume mmoja raia wa nchi jirani ya Malawi kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali, ambazo ni meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 155 za Kitanzania.
Tukio hilo lilitokea Februari 16, 2025, majira ya saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Msia, Kata ya Chitete, Wilaya ya Ileje.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 17, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alisema mtuhumiwa huyo, Chisamba Siame Kameme (60), raia wa Malawi, alikamatwa kupitia operesheni za kiintelijensia, misako, na doria zinazoendelea kwa ushirikiano na Idara ya Wanyamapori Wilaya ya Ileje.

Kwa mujibu wa Kamanda Senga, alisema tathmini ya awali ya wataalamu imebaini kuwa meno hayo, vipande 18 vyenye uzito wa kilo 84.2, yana thamani ya shilingi 155,311,020, sawa na Dola 60,000 za Marekani.
Aidha, Kamanda Senga alifafanua kuwa, meno hayo yametokana na tembo watatu, ambapo thamani ya tembo mmoja inakadiriwa kuwa takribani shilingi milioni 51.7.
Kamanda Senga alieleza kuwa mtuhumiwa alikutwa na meno hayo yakiwa yamefungwa kwenye baiskeli yake rangi nyeusi ndani ya mfuko wa sandarusi kwa lengo la kuyauza.
Kamanda Senga alisema kwa sasa, mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewaonya vikali watu wanaojihusisha na ujangili wa wanyamapori kuacha mara moja, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu.

More Stories
Makamba aahidi kumpigia kampeni Dkt.Samka kwa wazee
Bilioni 3 kukamilisha ujenzi shule amali Kata ya Choma
Serikali yatoa fursa kwa wahitimu kidato Cha nne 2024 kubadilisha Tahasusi