Na Esther Macha, Timesmajira,Online ,Mbeya
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Ushauri (RAAWU), Winston Makere ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi katika kutatua changamoto zinazojitokeza mara kwa mara mahali pa kazi .
Makere amesema hayo jana wakati akisoma risala ya ufunguzi kwa mgeni rasmi wakati wa semina ya siku tano kwa viongozi na wawakilishi wa matawi ya vyama vya wafanyakazi ambayo inafanyika mkoani Mbeya katika ukumbi wa chuo cha Uhasibu Mbeya .
Katibu huyo Makere amesema chama hicho kina wanachama 10,000 nchi nzima na kiutendaji kimegawanyika katika ngazi tatu, ambazo ni Tawi, kanda na Taifa.
Amesema kijiografia wana kanda tano ambazo ni Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Zanzibar, Kanda ya Kaskazini ni Mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kwamba kanda ya kati ina Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Singida,Tabora, na Kigoma
Aidha Makere ametaja Kanda ya Ziwa kuwa ina mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera,Shinyanga, Geita na Simiyu, kanda nyingine ni Nyanda za Juu Kusini ambayo mikoa yake ni Mbeya, Ruvuma ,Iringa, Rukwa,Songwe, Njombe na Katavi.
“Ndugu mgeni rasmi tunaamini taasisi yako ni mhimili unaojitegemea, hivyo tunaomba iendelee kutunga sheria ambazo ni rafiki kwa wafanyakazi na Taifa kwa ujumla,“amesema Makere.
Akizungumzia kuhusu changamoto Katibu Mkuu huyo amesema baadhi ya waajiri kutopenda uwepo wa chama mahali pa kazi hali inayopelekea uvunjifu wa haki za wafanyakazi, kutokuwepo kwa chombo kimoja kinachodhushulikia migogoro ya wafanyakazi mfano watumishi wa umma mchakato wao ni tofauti na watumishi wa sekta binafsi.
Akifungua semina hiyo siku tano kwa wawakilishi wa matawi ya vyama vya wafanyakazi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya, Dkt. Tulia Ackson amesema viongozi lazima wajue namna ya kutunza fedha wanazopokea kwa waajiri, kwani siku zote fedha huwa hazitoshi .
Aidha Dkt. Tulia amesema kuna changamoto kwa waajiri kuendelea kupata elimu hiyo itasaidia wafanyakazi wakiwa na sehemu ya kusemea matatizo yao.
Hata hivyo Naibu spika huyo amepongeza wanawake ambao ni viongozi wa matawi ya wafanyakazi na kuwataka kufanya kazi kwa uaminifu na nidhamu na bidii na wale walio nyuma yao kuwaamini waone kuwa wamefanya njia sahihi ya kuwachagua wanawake.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi