Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imesema utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni muhimu na kuzingatia ili kufanikisha utekelezaji kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa Oktoba 15, 2025 kijiji cha Ruvula mkoani Mtwara na Mjiolojia Mwandamizi kutoka PURA, Ebeneza Mollel, wakati wa zoezi la utoaji wa elimu ya mradi wa uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotarajiwa kutekelezwa katika kitalu cha Mnazi Bay kilichopo mkoani humo.

Mollel amesema,pamoja na kudhibiti shughuli za kitalaamu pia PURA inahakikisha wananchi wanajengewa uelewa wa miradi kabla ya kuanza utekelezaji.
“Sisi kama mamlaka tunahakikisha jamii zinazoishi au zinazozunguka maeneo ambayo miradi ya mkondo wa juu wa petroli inatekelezwa, zinashirikishwa kikamilifu na kujengewa uelewa wa kina kuhusiana na mradi husika,”amesema Mollel.
Pia amesema,PURA inafuatilia kwa karibu hatua zote za utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia na kuwakumbusha watekelezaji wa mradi huo umuhimu wa kuwajengea uelewa wananchi.
Zoezi la kuwajengea uelewa wananchi juu ya mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay,linafanyika katika vijiji vitatu ambavyo ni Ruvula, Msimbati na Mtandi vilivyopo Kata ya Msimbati mkoania Mtwara.
Mradi huo unaohusisha uchimbaji wa visima viwili vya uzalishaji na kisima kimoja cha utafiti unatarajiwa kugharimu zaidi ya dola za kimarekani milioni 80.2 unatekelezwa na kampuni ya Maurel et Prom Tanzania kwa kushirikiana na TPDC.

Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba 2025 ambao utawezesha ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 30 kwa siku.
Ongezeko hilo litasaidia upatikanaji wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme kwenye viwanda,nyumbani na kwenye vyombo vya usafiri kama magari na bajaji.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi