March 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PURA yaendelea kunadi vitalu 26 vya gesi asilia,mafuta

Na Penina Malundo,Timesmajira

MKURUGENZI  Mkuu wa Mamlaka  ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema wanaendelea kuvinadi vitalu 26 vya gesi asilia na mafuta ambapo kati ya hivyo Vitalu 23 vinapatikana katika Bahari ya Hindi, huku vitatu vikiwa katika Ziwa Tanganyika.

Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam Mhandisi Sangweni wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano 11 na maonesho ya Petroli nchi Wanachama Afrika Mashariki (EAPCE’25) alisema lengo la kunadi vitalu hivyo ni  kuvutia wawekezaji ili kuchangia maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Amesema mpango wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuweka nguvu zaidi katika suala la utafutaji wa mafuta na gesi hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inahamasisha nishati safi ya kupikia.

 “Kwa Mwaka huu kwetu ni muhimu kwani Kati ya shughuli wanazofanya ni kunadi na kuhamasisha uwekezaji katika tasnia ya utafutaji wa mafuta na gesi.

“Kwa kuanzia PURA tayari tuna maeneo hayo ambayo tumeyawekea misplaced ili kuweza  kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza na kuanza shughuli hizo,”amesema.

Aidha amesema kama watu wanavyofahamu Tanzania imegundua gesi kiasi cha futi za ujazo Trilioni 57.54 na katika gesi hiyo kiasi ambacho wamekwisha kihakiki ni Trilioni 1.16, na kwamba kazi zinazoendelea ni kuzihakiki hizo zilizogundulika kuwepo.

“Hata hivyo kiasi hicho cha Trilioni 1.16 tumeanza kukitumia mwaka 2004 kwa miradi kama ya kuzalisha umeme ikiwemo ya Ubungo, kwa kipindi chote hicho tumetumia Bilioni 800 hivyo kwenye Trilioni moja tumetumia hiyo Bilioni 800 unaweza kuona ni kiasi gani cha gesi kimegundulika,” amesema na kuongeza

“Sisi kazi yetu ni kutafuta mafuta hatutafuti gesi, gesi tumekuja kuipata katika utafutaji wa mafuta na Kati ya vitalu tutakavyokwenda kuvinadi ni vile vya Ziwa Tanganyika na viashiria vinaonesha kwamba ziwa hilo ambalo limepitiwa na bonde la ufa linauwezekano mkubwa wa kuwa na mafuta,” amesisitiza