Na Mwandishi wetu,timesmajira,Online
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),imesema itaendelea kutoa elimu kwa Watanzania na wawekezaji mbalimbali juu ya fursa ya sekta ya petroli nchini.
Akizungumza hayo leo Visiwani Zanzibar,katika maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanaendelea visiwani humo huku PURA ikiwa miongoni mwa taasisi zinazoshiriki,Mjiolojia wa PURA, Ebeneza Mollel,amesema PURA imejipanga kuwafikia wananchi na kuendelea kutoa uelewa wa masuala yahusuyo sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania pamoja na fursa zilizopo kwenye sekta husika.
Amesema uelewa huo kwa jamii utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli na hivyo kuongeza tija kiuchumi kwa taifa kuanzia ngazi ya mwananchi mmoja mmoja.
“Moja ya majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ni kuhakikisha inasimamia ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli, hivyo maonesho haya ni moja ya njia za kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa wa namna bora ya kuwa sehemu ya shughuli hizo,” amesema.
“Natoa wito kwa Watanzania wote watakaoweza kufika kwenye maonesho haya kutembelea banda la PURA ili kufahamu fursa zinazopatikana kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini pamoja na namna bora ya kupata fursa husika,” amesema
Kwa upande wake, Mjiolojia Faustine Matiku amesema tofauti na kutoa uelewa wa masuala ya fursa na ushirikishwaji wa wazawa kwenye sekta, watakaotembelea banda la PURA watapata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya mnyororo wa thamani katika sekta ya mafuta na gesi, utafiti na uzalishaji unaoendelea kwenye vitalu mbalimbali nchini, hali za leseni za utafutaji, mradi wa usindikaji gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG) na masuala mengine ya kiufundi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa