November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF yatwaa Tuzo ya Muwasilishaji Bora Taarifa za Mahesabu 2020

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dsm

Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Beatrice Musa-Lupi (kulia) na Grace Kabyemela, Mhasibu Mkuu wa PSSSF wakionyesha tuzo hiyo. Na Mpigapicha Wetu

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetwaa tuzo ya umahiri katika uwasilishaji  wa taarifa za hesabu kwa mwaka 2020.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo katika hafla ya kufunga mafunzo pamoja na utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Uandaaji wa Taarifa za Fedha za mwaka 2020 (Best Presented Financial Statements for the Year 2020 Awards) kwa taasisi, makampuni pamoja na mashirika zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) zilizofanyika katika hotel ya APC Bunju jijini Dar es Salaam Desemba 3, 2021, Mkurugenzi wa Fedha, PSSSF, Beatrice Musa-Lupi amesema ushindi huo ni ishara ya kwamba PSSSF inaandaa mahesabu kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa kimataifa lakini pia inaashiria uwepo wa weledi wa tasnia husika kwa upande wa watumishi.

“Sambamba na hayo niliyosema pia inaashiria uwepo wa usimamizi makini wa fedha za wanchama na hii inatupatia  heshima kama taasisi.” Amesema Mkurugenzi huyo wa Fedha PSSSF.

Musa-Lupi amewahakikishia wanachama wa mfuko huo kuwa dhamira ya PSSSF ni kuwahakikisha usalama wa michango yao huku ikizingatiwa kwa kiwango cha juu wakati wote, ikiwa ni pamoja na kuwepo uwazi kwenye usimamizi na utunzaji wa rasilimali za mfuko.

“Ushindi huu pia unaashiria uwepo wa kesho ya wanachama wetu kama kaulimbiu yetu inavyosema   ‘Leo. Kesho. Pamoja’.” Alihitimisha Beatrice Musa-Lupi

Washindi wa kwanza wa tuzo zilizotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu. Na Mpigapicha Wetu