April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSC kuendelea kuzijengea uwezo taasisi za umma

Na Mwandishi Maalum, PSC

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amesema Tume ya Utumishi wa
Umma itaendelea kuzijengea uwezo Taasisi za Umma na wadau kuhusu uzingatiaji wa
Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, ili ziweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo
Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa
Umma.

Mheshimiwa Mchengerwa amesema hayo jana wakati akiwasilisha taarifa kuhusu
utendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma kwenye Kikao cha Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), kilichofanyika Ofisi za Bunge jijini
Dodoma.

“Ili kuhakikisha malengo ya kuimarisha Utawala Bora yanafikiwa, Tume hupokea na
kutolea uamuzi rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma na kufanya ukaguzi wa
Uzingatiaji wa Masuala ya Rasilimali Watu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka
za Nidhamu katika Utumishi wa Umma. Aidha, Tume itaendelea kuzijengea uwezo
Taasisi za Umma na Wadau ili waweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo Sheria,
Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa
Umma,” amesema Mheshimiwa Mchengerwa.

Akizungumzia Mamlaka ya Tume amesema, ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake
katika Utumishi wa Umma, miongoni mwa Mamlaka ya Tume ni kuwachukulia hatua
kupitia mamlaka zao za nidhamu watendaji wakuu wanaoshindwa kuwachukulia hatua
watumishi walio chini yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia
utendaji kazi katika Utumishi wa umma.

Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za
Mitaa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Abdallah Jafari
Chaurembo (Mb) walisema, bado kuna tatizo kwa baadhi ya Waajiri, Mamlaka za Ajira
na Mamlaka Nidhamu katika utekelezaji wa maagizo ya tume.

“Watumishi wa umma waliosimamishwa au waliofukuzwa kazi na Waajiri au mamlaka
zao za Nidhamu na kukata Rufaa Tume, pale inapoamuliwa na Tume na kuagiza
warejeshwe kazini na shauri lianze upya tafsiri imekuwa ngumu katika utekelezaji wa
maagizo ya Tume namna ya kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa katika
kushughulikia na kuhitimisha mashauri ya Nidhamu,”amesema.

Wajumbe wa kamati hiyo muhimu ya Bunge walisisitiza umuhimu wa matumizi ya
TEHAMA kutekelezwa ipasavyo majukumu ya msingi ya tume ili kuiwezesha tume
kushughulikia rufaa na malalamiko mengi na kufanya ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa
ufanisi zaidi.