December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Promota afunguka sababu za Mfaume, Maono ‘kulimwa’ asilimia 20

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

PROMOTA Mikhaylov Maxim kutoka nchini Urusi amefunguka sababu za kukata asilimia 20 ya pesa walizopaswa kupewa mabondia wa nchini Tanzania Mfaume Mfaume na Maono Ally waliopoteza mapambano yao nchini humo mwshoni mwa wiki iliyopita.

Mfaume alipoteza pambano hilo kwa kupigwa Tencnical KnockOut (TKO) ya sekunde ya kwanza katika raundi ya pili dhidi ya bondia Rizvan Elikhanov huku Maono kutika Kiwangwa, Bagamoyo akipoteza pambano lake raundi ya kwanza.

Akizungumza na Mtandao huu, Maxim amesema kuwa, ameamua kukata asilimia hiyo 20 ya pesa sawa na dola 1,000 alizopaswa kuwalipa mabondia hao kutokana na mambo waliyoyafanya ulingoni wakati ni wazi walionekana wana uwezo wa kuendelea na pambano.

Awali wakitaka kukata fedha nyingi zaidi lakini walishauriwa kuwa mawakala wa mabondia hao walikuwa wameshatumia gharama kubwa katika maandalizi, vipimo vya Covid 19, kipimo cha MRI, kipima kundi lake la damu pamoja na gharama nyingine.

Amesema, jambo hilo linadhihirisha kuwa mabondia hao walikwenda kwa ajili ya kufata pesa na si kutoa ushindani kwani hakuna bondia yoyote kati ya hao wawili aliyepigwa ngumi ya maana iliyomfanya kushindwa kuendelea na pambano.

“Ukiangalia kwa jinsi mabondia hawa walivyocheza walikuwa wakionekana kuwa wana uwezo wa kuendelea na hata video niliyokutumia inaonesha wazi jinsi bondia alivyokuwa anajiangusha hivyo tayari tumeshaiwakilisha kwa Shirikisho linalosimamia ngumi nchini mwetu kutumika kama ushahidi wa ushahidi kwa Shirikisho linalosimamia ngumi nchini mwao,” amesema Maxim.

Promota huyo amesema, anaamini kuwa kilichomfanya mchezaji huyo kutoka mchezoni na kukubali kupigwa TKO yawezekana ni hofu ya kuumia kwani alisema hawezi kuendelea kwakuwa ameumia bega licha ya kuwa hakuna ngumi yoyote aliyopigwa eneo hilo wala yeye kurusha ngumi.

“Watu wa karibu wa bondia huyu wametueleza kuwa hivi miezi michache iliyopita alikuwa na pambano Dubai ambalo aliumizwa kichwa na kulazwa karibu wiki hivyo huenda aliingia ulingoni na hiyo hali na kuhofu kuwa akiendelea na pambano huenda yakamkuta hayo,” alisema Maxim.

Mara baada ya kuwasili hapa nchini akitokea Urusi, Mfaume aliweka wasi kuwa, kilichomfanya kupoteza pambano hilo ni baada ya kutoka mchezoni kutokana na kutokuwana maandalizi ya kutosha.

Lakini pia amedai kuwa, pia hakujua kuwa mpinzani wake alikuwa na kilo 72 na yeye zake ziliandikwa 71 wakati kiuhalisia uzani anaopigana ni kilo 69 na hicho ni kielelezo tosha kuwa taratibu nyingi zilikiukwa katika pambano.

Licha ya kutambua kuwa hakua na sawa na taratibu nyingi kukiukwa lakini bado bondia huyo alipanda ulingoni kwa ajili ya pambano na kudai kuwa muandaaji wa pambano aliwakata asilimi 80 baada ya kupoteza ambazo za zaidi ya milioni sita na kupewa asilimia 20 ambazo ni sawa na milioni 2.

Kwa upande wake mmoja wa viongozi kutoka Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi amesema kuwa, yeye kama kiongozi ametumiwa vielelezo vyo ambavyo vinaonesha Mfaume alisaini pambano la kilo 74 na si 72 kama anavyosema yeye.

Amesema kuwa, pia kiasi ambacho walikatwa mabondia hao ni asilimia 20 kwa jambo walilofanya lakini pia licha ya waandaaji wa pambano hilo kutokuliweka mtandaoni pambano zima lakini wametumiwa baadhi ya vipande ambavyo ni kama ushahidi wa kile kilichofcanywa na mabondia hao ulingoni.

Kiongozi huyo amesema kuwa, pia tayari wameshawatumia barua mabondia hao ili kwenda kujieleza kile kilichotokea na leo Jumatatu huenda wakakutana na viongozi ili kuzungumzia jambo hilo.

Mbali na sakata hilo, kiongozi huyo aliwataka mabondia wa Tanzania kuacha kutengenezab rekodi ili waonekane bora kimataifa wakati wengi wao wanataka kupigana na watu ambao hawajacheza muda mrefu au wanaotoka kambi moja.