Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
Serikali imezindua Awamu ya Sita ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP VI) iliyolenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato ya ndani pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma katika Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Saada Salum Mkuya amesema, utekelezaji wa programu hiyo unafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Wadau wa Maendeleo.
“Lengo la Programu hii ni kuhakikisha kunakuwa na usimamizi imara wa ukusanyaji wa mapato na urasimishaji wa sekta zisizo rasmi ili kupata mchango wao kwenye ukusanyaji wa mapato hayo.”amesema Dkt.Mkuya na kuongeza kuwa
“Katika kuhakikisha utekelezaji wa Programu hii,Serikali itazijengea uwezo taasisi zote zinazohusika na masuala ya usimamizi wa matumizi ya umma zikiwemo taasisi za ukaguzi na Bunge ili kuzuia mianya yote ya ufujaji wa fedha za umma na kuongeza uwazi na uwajibikaji”.
Kwa mujibu wa Waziri huyo,Programu hiyo pia imehusisha masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yatasimamiwa kuanzia wakati wa uandaaji na utekelezaji wa bajeti.
Akizungumza katika hafla hiyo,Mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo, Milou Vanmulken, ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania kuweza kutekeleza programu mbalimbali zilizopita ambazo changamoto zake zimewezesha kutengeneza programu mpya ambayo utekelezaji wake utaongeza ufanisi na uwajibikaji katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
Awali Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Denis Mihayo amesema Programu za Usimamizi wa Fedha za Umma zimeanza tangu miaka ya 90 kwa awamu tofauti za miaka mitano mitano ambapo kila baada ya awamu kumalizika hufanyika tathmini ambazo matokeo yake husaidia kuanzisha awamu nyingine ili kutatua changamoto zilizojitokeza katika awamu iliyotangulia.
“Mafanikio ya awamu zilizopita ni kuanzishwa kwa mifumo mbalimbali ya ukusanyaji mapato kama vile GePG kwa Tanzania Bara, Zan Malipo kwa Zanzibar na TAUSI unaotumiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.”amesema Mihayo
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano