Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline
,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema ameridhika na ufanyaji kazi wa vijana wa Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kwa kuweza kuyafikia malengo ya Serikali na wao wenyewe kwa kuwa na miradi ya ufugaji na uvuvi.
Ni baada ya Agosti 2, 2024 kutembelea mabanda ya vijana hao kwenye Maonesho ya Nanenane ya kitaifa na kimataifa yanayofanyika jijini Dodoma na kujionea shughuli wanazofanya ikiwemo ufugaji na uvuvi.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea mabanda ikiwemo yale ya halmashauri za mikoa ya Kanda ya Kati Dodoma na Singida,Sekta Binafsi na Vijana wa BBT, amesema ameridhika na kazi zinazofanywa na wadau mbalimbali kwenye masuala ya mifugo na uvuvi.
“Nimeweza kutembelea mabanda ya mifugo na uvuvi na nimeweza kutembelea mabanda ya Private Sector (Sekta Binafsi) na nimeweza kutembelea sehemu ya vipando (mashamba darasa) ambapo wenzetu wa Wizara ya Kilimo wamepanda kule, lakini mwisho nimetembelea hapa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kwanza nimefurahi kuona taasisi zetu za mifugo na uvuvi wanavyofanya kazi kule,wameonesha vitu vingi wanavyofanya.
“Lakini pia tumeweza kuona katika mambo makubwa yanayofanyika ni suala la vijana wa BBT. Tumeona pale vijana wetu wa BBT ya mifugo na BBT ya uvuvi ambao walipata elimu nzuri ya namna ya ufugaji na unenepeshaji wa mifugo na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na tumefarijika wao wenyewe wakitoa ushuhuda namna walivyofundishwa namna walivyoingia mikataba na NARCO kupewa maeneo ya ardhi kwa muda wa miaka mitano” amesema Prof. Shemdoe.
Profesa Shemdoe amesema hata wale BBT ya Uvuvi nao wameeleza namna walivyopewa mikopo iliyowasaidia kufanya shughuli zao za uvuvi kwa kutumia vizimba na wameridhika na kazi waliyoifanya, lakini pia wameonesha kilimo cha malisho na kazi nyingine wanazofanya.
Profesa Shemdoe amesema kuwa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anafungua maonesho hayo Agosti Mosi, 2024 alisema maana ya maonesho hayo ni wakulima kwenda kuchukua teknolojia ya kilimo, mifugo na uvuvi na kweli walivyotembelea kwenye banda la mifugo wameona teknolojia hiyo.
“Ninyi wenyewe ni mashuhuda hapa, pale awali wakati tunaingia hapa kuna ndugu zangu wamasai walifika kuona mifugo na teknolojia inayotumika wamesema ni kweli kuna tofauti kati ya mifugo hii na ile ya kwao, hivyo watakwenda kuwaeleza wenzao nao wafike hapa kuona, pia waone namna na wao kuboresha mifugo yao.
“Nitoe wito kwa watanzania wenzangu, wana Dodoma mliopo Dodoma hii, hebu tumieni muda wa hizi siku nane kuja kujionea teknolojia mbalimbali ambazo zipo hapa, nadhani mtu ataondoka na kitu ambacho kitamsaidia sana,Wakuu wa Wilaya niwaombe sana, mkizungumza na wananchi wenzetu, muwasisitize wafike hapa, wote tumejionea kuna watu wametoka nje ya nchi kuja kujionea maonesho haya” amesema Prof.Shemdoe.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja