September 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Ndakidemi:Vijana wapatiwe mafunzo kabla ya kupewa mikopo

 Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma 

SERIKALI imesema kuwa  katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya vijana 2,685 walipatiwa mafunzo ujasiriamali mikoa ya Dodoma, Kagera, Manyara, Kigoma, Shinyanga, Mwanza na Arusha kabla hawajapatiwa huduma za mikopo.

Hayo yamesemwa  bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),Patrobas  Katambi wakati  akijibu swali la mbunge wa Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi .

Katika swali lake,Profesa Ndakidemi alitaka  kujua kwamba Serikali inatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa kiasi gani kwa vijana kabla hawajapatiwa huduma za Mikopo toka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Katambi amesema kuwa ili kuwaandaa vijana kabla ya kupatiwa mikopo, Vijana hao wamekuwa wakipatiwa mafuzo ya Ujasiriamali, Uanzishaji wa Miradi, Usimamizi na Uendelezaji na Urasimishaji pamoja na pia kuunganishwa na huduma wezeshi kupitia Taasisi za fedha na Benki, Mamlaka za Kodi, Mamlaka za uendelezaji viwanda vidogo vidogo (SIDO); Huduma za uthibiti usalama na viwango Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), na huduma za hifadhi ya jamii.

Katika maswali yake ya nyongeza Profesa Ndakidemi aliihoji Serikali kwa nini isitenge fedha za kutosha na kuziweka katika mfuko huo ili zisaidie vijana hao katika kutatua changamoto ambazo wanakabiliana nazo huku akisema  Vijana ni nguzo muhimu katika Taifa. 

Pia alitaka kujua “Je Kuna mfumo gani wa kufuatilia vijana wanaopata fedha katika mfuko huo,kuangalia kama wamepata changamoto, mafanikio gani kutokana na fedha wanaozipatiwa kutoka mfuko huo wa Maendeleo ya Vijana?

Akijibu Naibu Waziri Katambi amesema kuwa kuna umuhimu ambao waliuona kama serikali kupitia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba kundi la vijana ndio nguvu kazi kwa mujibu wa sensa ambayo yalipatikana.

Kwa mujibu wa Katambi , Dkt.Rais Samia alihakisha kila Wizara inatengewa fungu maalum kwa ajili  ya shughuli za vijana na kwamba kwa kuanza ilianza na ofisi ya Waziri Mkuu ambapo walipatiwa bilioni 1 kila mwaka wa fedha kuhakikisha vijana hao wanakopeshwa.

Waziri huyo alieleza kuwa Wizara ya Madini ambayo imeanzisha programu ya Mining  Better  Tomorrow ambayo inalenga katika kuwasaidia vijana wachimbaji wadogo wadogo na kuwawezesha kimtaji hivyo hivyo na Wizara ya michezo.

“Wote watanzania mnaushahidi Rais Dk. Samia kupitia Bunge hili zimekuwa zikipitishwa fedha kwa ajili ya kuwakopesha vijana waliokwenye kazi za sanaa lakini pia hata kwenye michezo timu zetu zimekuwa zikipata mkono wa mama kwa namna mbalimbali timu za  Simba na Yanga zimekuwa zikinufaika na fedha hizi,” amesema na kuongeza kuwa

” Wizara ya kilimo nayo ina program maalum ya Building Better tomorrow kwa ajili ya vijana na kwamba wanaenda kutenga ya trillioni 1 ambapo wanaufaika ni vijana hao.”

Amesema kila Wizara zimewekewa fedha na kwamba waliona kuziweka katika kapu moja hauwezi kuwasaidia kwa pamoja lengo ni kuweka katika Wizara za kisekta ili kuwafikia wengi zaidi.

Akijibu swali la pili la mbunge huyo amesema wanafuatilia na kuwajengea uwezo kabla ya kuwakopesha pamoja na kufanya thamini ili kuona waliombea fedha hiyo na kuwasimamia.

Waziri huyo alisema lengo ili waweze kujitegemea, kujiaijri  na kuweza kuchangia katika Pato la Taifa na kwamba serikali ya awamu ya sita inaheshimu vijana kwa kuwa ndio nguvu kazi ya Taifa kwa sehemu kubwa.