January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo kufanya mkutano wa dharura kujadili ufunguzi Sekondari ya Nyasaungu

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoa wa Mara Prof.Sospter Muhongo anatarajia kufanya Mkutano wa dharura na Wananchi wa Kijiji cha Nyasaungu kilichopo  kata ya Ifulifu Jimboni humo kwa lengo la kujadili maandalizi ya ufunguzi wa Sekondari ya Nyasaungu.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo Disemba 2, 2024. Ambapo mkutano huo , umetayarishwa  na Mbunge huyo na umepangwa kufanyika Disemba 7, 2024 Kijijini Nyasaungu Senta.

“Azimio la Wa-Nyasaungu la  Jumatatu,   Disemba 2,  2024, ni  Sekondari ya Nyasaungu  ifunguliwe Januari 2025. Azimio hili limetolewa  wakati wa maziko ya Marehemu Steven Chacha Mwita Wambura (1955-2024) aliyekuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa uchangiaji wa ujenzi wa Nyasaungu Sekondari.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ambapo Waombolezaji mbalimbali walihudhuria  akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka, Katibu Tawala wa Wilaya ya Musoma Ally Mwendo, Wananchi wa Nyasaungu,  Vijiji jirani,  marafiki, ndugu, pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Sospter Muhongo.

Aidha taarifa hiyo imesema, Wana-Nyasaungu wameamua kumuenzi Marehemu Steven Chacha kwa michango yake inayotambulika Kijiji Nyasaungu ikiwemo ya ujenzi wa Shule ya Msingi  Nyasaungu, Nyasaungu Sekondari na Zahanati ya Kijiji cha Nyasaungu (inafungulia wiki ijayo).

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amewashukuru Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini na Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuendelea kushirikiana katika suala la maendeleo jimboni humo. Huku pia akiahidi kushirikiana nao kwa dhati katika kusikiliza na kutatua kero zao.

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha  Nyasaungu akiwemo Maira Jacob amesema kufunguliwa kwa shule hiyo kutaongeza wigo kwa wanafunzi kusoma karibu na kwao, huku pia  akimshukuru Mbunge Pro. Muhongo  na Serikali kwa kuendelea Kuimarisha sekta ya elimu jimboni humo.