Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
SERIKALI imekanusha uvumi unaosema kwamba kufuta kutangaza shule bora ni kwa sababu inaogopa ushindani dhidi ya shule zake na shule binafsi .
Aidha imesema itaendelea kuzifungia shule ,vyuo,kuwafutia mitihani na kuwachukuliwa hatua watu wote watakaojihusisha na udanganyifu wa mitihani bila kujali muhusika kama anatoka serikalini au sekta binafsi.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameyasema hayo jana Bungeni Jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 ya maombi ya shilingi trilioni 1.675 ambayo ilipitishwa na Bunge.
Amesema,serikali iliamua kufuta kutangaza shule na mwanafunzi bora kwa sababu maalum zilizoelezwa na wataalam lakini siyo kwa sababu serikali inaogopa ushindani na shule binafsi.
“Yaani shule binafsi ni washindani wa serikali ,narudia tena,yaani wizara inaona shule binafsi,vyuo binafsi ni washindani ,never,hapana,haijawahi kutokea na haitatokea na haiwezi kutokea chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ,haitatokea hata baadaye ,hii ni serikali ya wananchi na hizi shule zinafundisha watanzania.”amesema Profesa Mkenda
Hata hivyo amesema kwa wale wanaoataka kutangaza, matokeo yapo hadharani lakini kwa upande wa serikali haiwezi kufanya hivyo tena kwa vigezo ambavyo wanataaluma wenyewe wamevikataa.
Amesema,shule pamoja na vyuo vikuu binafsi vimekuwa msaada sana hapa nchini kwani imewaondolea watanzania adha ya kupeleka watoto kwenda kusoma nje ya nchi.
“Zamani tulikuwa tunaona watoto wetu wadogo wanaondoka wanaenda kusoma Kenya, wanaenda kusoma Uganda, leo shule zimetufuata nyumbani tunazifurahia,hata siku moja Serikali haiwezi kusema kwamba hizo ni shule shindani dhidi yake,
“Inachoweza kufanya ni kuzilinda ,kuzitetea na kusema ukweli kwamba tumekutana mara nyingi na wamiliki wa sekta binfasi na tukaongea na bado tutandelea kufanya hivyo kwa maelekezo ya Rais wetu kwa mustakabali wa elimu yetu hapa nchini.”
Amesema,Serikali imeamua kushindanisha wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwa vigezo vinavyokubalika na kuwapa ufadhili kupitia mkopo wa Samia Scholarship na katika hilo hatujawagawa wanafunzi wanapata hadi wa shule binafsi ili mradi tu amekidhi vigezo.
Kuhusu kufungia shule zikiwemo za binafsi amesema,zinaonekana kama ni zenyewe tu ndiyo zinafungiwa ni kwa sababu zimekuwa zikionyesha mfumo wa shule nzima kujihusisha kwenye udanganyifu wa mitihani.
Akijibu hoja ya wabunge waliotaka kujua kwa nini Serikali inakuwa na haraka ya kufungia shule binafsi huku wakitolea mfano shule ya Olimpio ambako walida kulikuwa na wizi wa mtihani Profesa Mkenda amesema, shule inayofungiwa kuwa kituo cha mtihani ni ile inayoonyesha mfumo wa kitaasisi wa udanganyifu wa mitihani na siyo mwanafunzi mmoja mmoja.
“Kwenye suala la udanganyifu wa mitihani ,wanafunzi wote wanaohusika na udanganyifu huo tunafuta matokeo haijalishi anatoka shule ya umma au anatoka shule binafsi ,
“Lakini shule inayofungiwa kuwa kituo cha mitihani ni shule ambayo tumeona kulikuwa na ‘organized effort ya kucheat’ ndani ya shule, (mfumo wa kitaasisi wa kufanya udanganyifu ndani ya shule) siyo mwanafunzi mmojammoja maana hata zile shule binafsi ambazo unakuta mwanafunzi mmoja mmoja amecheat hatuzifungii.”
“Mfano ipo shule moja ambayo mlisikia binti mmoja analalamika namna alivyobadilishiwa namba ya mtihani na kurudishiwa namba yake katika mtihani wa mwisho na kupewa onyo na walimu kwamba wasiseme kilichotokea,na sisi tulitumia malalamiko yake kufanya uchunguzi tukagundua kwamba yalikuwa ni ya ukweli ,
“Na shule hiyo ilikuwa ni miongoni mwa shule bora,na iliongoza kwenye mkoa husika ,sasa hapo siyo kwamba mwanafunzi kafanya udanganyifu lakini walimu wameshirikiana wamebadilisha namba za mtihani halafu wanawaita wanafunzi wanawaambia msiseme ,shule hiyo tumeifunga kama kituo cha mitihani na wahusika wote wakiwemo wa serikali na binafsi wamechukuliwa hatua za kisheria.”
Alitolea mfano mwingine wa mwanafunzi ambaye aliingia na simu ya mkononi katika chumba cha mtihani huku akijua dhahiri hairuhusiwi amesema mwanafunzi huyo alitumia simu hiyo kupiga picha mitihani na kumtumia mwenye shule ambaye alipanga watu wa kuandika majibu.
“Sasa huyo hafai kutetewa,sekta binafsi mnafanya kazi nzuri sana msitetee vitendo kama hivi,kwa hiyo serikali iatendelea kuwafungia wanafunzi wanaofanya udanganyifu pamoja na shule lakini pia kuwachukulia hatua watu wote waliohusika kwenye usimamizi wa mitihani katika shule husika.”amesisitiza Profesa Mkenda
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best