Na Mwandishi wetu,timesmajira,Mtwara
WAZIRI wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda amewataka wabanguaji zao la korosho kuja na mikakati itakayowezesha zoezi hilo kufikia asilimia 60 au 100 ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkenda ameyasema hayo mjini Mtwara wakati akizungumza na wadau wa ubanguaji Korosho kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mkoani hapo.
Amesema kuwa madhumuni ya kikao hicho ni kushauriana kujenga mwelekeo wa kuhakikisha kwamba adhma inafikiwa ya walau kima cha chini ya asilimia 60 ya korosho ibanguliwe hapa nchini.
“Na hicho ni kima cha chini kabisa ikifika mwaka 2025 maana kima cha chini kabisa ni kwamba tukifika asilimia 100 tena ndio tutafurahi zaidi sasa kwa kasi ambayo tunakwenda nayo ni vizuri tukawa tunashauriana kwa maana 2025 ni kesho tuu,”amesema
Amesema kuwa kwa sasa ni asilimia 10 tu ya korosho inabanguliwa hapa nchini na ubora umeongezeka na ladha imekuwa nzuri zaidi lakini linahitajika soko kubwa la nje kwa kuwa fedha nyingi zipo huko.
“Tukiweza kuwauzia wale sababu kipato na fedha zipo huko nyingi, wakulima watakuwa na fedha nyingi zaidi na kutakuwa na ajira za kutosha nchini hasa maeneo ya Mtwara na Lindi na Serikali itapata fedha,”amesema
Amebainisha ni changamoto inayotakuwa kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau wote kwakuwa Serikali haiwezi kutekeleza yenyewe kwa kukaa ofisini.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa kilimo, Hussein Bashe amesema kuongeza thamani kwenye zao hilo ni jambo la msingi hususani kwenye ubanguaji.
Amesema zipo changamoto za riba kwenye zao hilo ambapo Rais ametoa Trilioni moja kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli za kiuchumi zitakazokopeshwa chini ya asilimia 10 na taasisi za fedha.
Amesema changamoto wanayokabiliana nayo wabanguaji ni mitaji kwamba kiwanda kina uwezo wa kuchakata tani 10 kwa siku maana yake kwa mwezi ni tani 300 hivyo ili kufanye kazi mwaka mzima kinahitaji zaidi ya tani 3,600.
Ameongeza kuwa zipo changamoto za kisera ambazo zimeshaanza kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za fedha ili wabangue korosho kwa kiasi kikubwa.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote