January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda akerwa watoto kuimba,kucheza wimbo wa Zuchu shuleni

Na Joyce Kasiki,Dodoma

WIZARA ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ameagiza kusimamishwa kazi kwa walimu wa shule mbili zilizopo katika wilaya ya Tunduma mkoani Songwe kutokana na kuruhusu watoto wanaosoma katika shule hiyo kuimba na kucheza wimbo wa Zuchu maarufu kama ‘honey’.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma Waziri Mkenda alisema,kitendo hicho cha watoto kucheza na kuimba wimbo huo ambao unakiuka maadili ambayo yamezoeleka hapa nchini.

“Tumebaini shule yenyewe ipo Tunduma ,kulikuwa na kikundi kimeenda kutoa msaada shuleni baada ya kutoa msaada ule kikaweka na muziki halafu wanafunzi nao wakauimba na kucheza .”amesema Prof.Mkenda

Profesa Mkenda amesema,shuleni ni sehemu ya malezi na kufundisha watoto maadili mema na kwamba watoto wawapo shuleni walimu ndio wanaotegemewa kusaidia wazazi katika suala la malezi yao.

“Kwa hiyo pamoja na kwamba muziki uliletwa na kikundi kutoka nje ya shule lakini muziki ukachezwa na walimu walikuwepo lakini hawakusitisha,tumeongea na wadhibiti ubora wapeleke taarifa kwa Mkurugenzi awaondoe walimu wakuu wa shule hizo mbili za Tunduma kwenye mamlaka ya ukuu wa shule na watafutwe wakuu wengine ,”alisistiza Prof.Mkenda na kuongeza kuwa

“Tunaomba walimu wakuu mtusaidie vitu kama hivi visiingie shuleni ,wazazi wanatulalamikia sana kwamba nyie mnaosimamia sekta ya elimu mnaachaje vitu kama hivi vinaingia shuleni ,na sisi tunatarajia kwamba mwalimu mkuu ukishaingia kule utatusaidia sisi kwamba unalimda maadili kulingana na matakwa ya  wazazi  ambao wametuletea watoto wao kuwalea.

“Kwa hiyo taarifa imeshaenda na tutafuatilia walimu wakuu shule hizo mbili wataondolewa ,tunajua tukio lilitokea Oktoba 6,mwaka huu lakini mpaka sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa maana hiyo kulikuwa na fursa hata kama mwalimu mkuu alikuwa hayupo angekuwa alishachukua hatua.”

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima alisema kuwa yeye  ni miongoni mwa Mawaziri wenye dhamana ya kufuatilia watoto katika sekta zote hasa inapokiukwa miongozo ya malezi na makuzi ya watoto.

“Kwa hiyo mimi popote pale ninapoona hapazingatiwi nitanyanyua sauti kwenda kwa waziri wa kisekta na hatua zitachukuliwa ,nawasihi  watoa huduma wote kwa watoto kwamba ,jukumu la malezi na makuzi ya watoto ni letu sote.”alisema Dkt.Gwajima

Kumekuwa na picha za video ambazo zinasambaa katika mitandao ya kijamii zikionesha watoto na baadhi ya watu wazima wakiwa shuleni wakiimba na kucheza wimbo wa zuchu unaofahamika kwa jina la honey ,kitendo ambacho kimetafsiriwa kuwa ni kinyume na maadili kwa watoto hao.