May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakandarasi watakiwa kutekeleza miradi REA bila kuichafua serikali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na uadilifu ili kuondoa malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi ambayo yanaweza kuichafua Serikali.

Ameyasema hayo leo wakati wa tukio la kusaini mikataba ya upelekaji umeme vijijini kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na B, lililofanyika katika Ofisi Ndogo za REA zilizoko jijini Dar es Salaam.

“Mwananchi anapokulalamikia wewe Mkandarasi, ujue anailalamikia Serikali, hivyo simamieni maadili na utendaji kazi sahihi wa wafanyakazi wenu vijijini,” amesisitiza.

Akitoa mfano, amesema yapo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa baadhi ya wafanyakazi wa Wakandarasi wamekuwa wakikata miti katika maeneo yao pasipo kuwapa taarifa, jambo ambalo amelikemea vikali akisema kamwe halikubaliki.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa kwanza kulia), akizungumza na Wakandarasi wakati wa tukio la utiaji saini mikataba ya kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na nyongeza ya Ujazilizi Fungu la Pili B, Ofisi Ndogo za REA jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023.

“Japokuwa miradi ya umeme vijijini haina fidia, lakini hiyo haiondoi haki ya mwananchi kwamba eneo ni la kwake. Hivyo, tunatarajia kutakuwa na mawasiliano na mahusiano mazuri kati yenu ninyi wakandarasi na wenye maeneo yao. Kabla hujakata mti, mfahamishe aelewe.”

Akieleza zaidi, Mhandisi Saidy ameainisha mambo mengine kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatiwa na kila Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kutimiza lengo maalumu la Serikali la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwafikishia huduma ya umeme.

Akifafanua kuhusu suala hilo, Mkurugenzi Mkuu amesisitiza kuwa Wakandarasi wote wanaoenda kufanya kazi vijijini wanapaswa kuzingatia kuwa wanafanya kazi hiyo wakiwa ni waajiriwa wa Serikali sawa na mikataba waliyosaini.

Aidha, amewataka kufanya kazi kwa ukaribu na viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali pamoja na Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi katika maeneo husika. Katika hili, amewataka kuhakikisha wanawajibika kwa viongozi hao kwa kuwapatia taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Vilevile amewaelekeza Wakandarasi hao kusimamia suala la weledi na uaminifu kwa wafanyakazi wao ili kuepusha vitendo vya rushwa pamoja na matumizi ya maneno yasiyo na staha kwa wananchi.

Amesema, REA inafuatilia kwa ukaribu na kuhifadhi taarifa zote za utendaji kazi wa Wakandarasi hivyo ikitokea yeyote kati yao akakataliwa kufanya kazi katika miradi itakayofuata ilhali utendaji kazi wake ulikuwa mzuri, ajue ziko sababu nyingine zilizomwondolea sifa ikiwemo hiyo ya uzingatiaji maadili.

Akifafanua zaidi kuhusu vitendo vya rushwa, Mhandisi Saidy amewataka Wakandarasi kuweka katazo kwa wafanyakazi wao kujihusisha na kazi za kutandaza mfumo wa nyaya za umeme (wiring) hata kama wana leseni bali wafanye kazi iliyowapeleka ambayo ni kujenga miundombinu ya umeme vijijini.

Katika hatua nyingine, amesema hakutakuwa na nyongeza ya muda katika utekelezaji wa miradi ambayo mikataba yake imesainiwa. Hivyo, kabla ya kusaini, alimtaka kila mmoja kujitafakari na kujiridhisha kama anao uwezo wa kutekeleza kazi hiyo ndani ya muda ulioainishwa katika mkataba.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa nchini Tanzania (AFD), Celine Robert, ambao ni mojawapo ya Wafadhili katika miradi hiyo, alisema Ufaransa inafurahishwa kuwa sehemu ya uchangiaji wa miradi inayosaidia kuboresha maisha ya kila siku ya wananchi na akaongeza kuwa watafarijika kuona wakandarasi wakitekeleza miradi hiyo kwa ufanisi.

Naye Mkurugenzi wa Umeme Vijijini kutoka REA, Mhandisi Jones Olotu amewasisitiza wakandarasi hao kufanya kazi kwa mujibu wa mikataba waliyosaini huku Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi Advera Mwijage akiwataka kuhakikisha wanawalipa vibarua wao kwa wakati pamoja na kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira.

Wawakilishi kutoka Kampuni ya Ukandarasi ya Derm Group (T) LTD (kushoto) wakitia saini mikataba ya kupeleka umeme vijijini wakati wa tukio la utiaji saini mikataba hiyo kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na nyongeza ya Ujazilizi Fungu la Pili B, lililofanyika katika Ofisi Ndogo za Wakala wa Nishati Vijijini (REA), jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria kutoka REA, Mussa Muze.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa niaba ya wakandarasi wenzao, Baltazary Masindi kutoka Kampuni ya Sengerema Engineering Group Ltd na Aymen Louhaichi kutoka STEG International Services wameshukuru kwa nafasi waliyopata na kuahidi kutekeleza miradi hiyo kwa weledi, uaminifu, viwango na ndani ya wakati ulioainishwa katika Mkataba.

Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Norway kwa gharama ya shilingi bilioni 263.3 ambapo utatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Mara, Manyara, Mtwara, Rukwa, Ruvuma na Simiyu.

Mradi huu utahusisha kupeleka umeme katika vitongoji 1,880, kujenga njia za umeme kilomita 5,640, kufunga transfoma 1,880 pamoja na kuunganisha wateja wa awali 94,000.

Kwa upande wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B, Mikataba miwili iliyosainiwa ni nyongeza ya mikataba iliyosainiwa mwezi Februari mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Miradi hii itatekelezwa katika Mikoa ya Kigoma na Geita kwa ufadhili wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo (AFD) kwa gharama ya shilingi bilioni 37.9

Mkurugenzi Mkuu wa REA, kwa niaba ya Serikali amewashukuru Wafadhili wanaoendelea kuchangia katika utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini wakiwemo Benki ya Dunia pamoja na Serikali za Ufaransa na Norway.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage akizungumza wakati wa tukio la utiaji saini mikataba ya kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili C na nyongeza ya Ujazilizi Fungu la Pili B, Ofisi Ndogo za REA jijini Dar es Salaam, Novemba 2, 2023.