Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
WAZIRI wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amezitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha ukamilishaji wa barabara zinazounganisha Kurasini Logistic Park ili eneo hilo lianze kutoa huduma ifikapo Januari 2027 na kusaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam
Prof. Mbarawa ametoa maagizo hayo Novemba 12, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kurasini Logistic Park.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa bandari kuhifadhi na kuhudumia shehena pamoja na kuimarisha ufanisi wa usafirishaji katika ukanda wa kikanda

Amesema mradi unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itakuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 150,000 na ya pili makasha 550,000 kwa mwaka, hivyo kufanya eneo lote kuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 700,000 kwa mwaka
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha ukaguzi wa makasha nje ya eneo kuu la bandari, ikiwemo uhakiki wa nyaraka na uchunguzi kwa kutumia vifaa maalumu vya kisasa vya kuskani.

Aidha, amesema mradi huo unatekelezwa kupitia uwekezaji wa sekta binafsi, huku mwekezaji akiwa pia na dhamana ya kuendesha Kituo cha Huduma za Makasha Namba Mbili (Terminal Two)
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam,Abed Gallus, amesema ongezeko la shehena limeongeza mahitaji ya maeneo ya kuhifadhi makasha. Ameeleza kuwa mwaka uliopita bandari ilihudumia zaidi ya makasha milioni 1.3, huku mwaka 2026 ikitarajiwa kuhudumia zaidi ya makasha milioni 1.5

Aidha, Gallus amesema eneo hilo litakuwa na vifaa vya kutosha vya kuskani na mifumo ya kisasa ya uhakiki wa makasha, hatua itakayowezesha baadhi ya shughuli za ukaguzi kufanyika nje ya bandari. Hatua hiyo itapunguza msongamano, kuongeza kasi ya upitishaji wa mizigo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wadau wa usafirishaji.

More Stories
Dkt.Mwigulu mgeni rasmi kilele miaka 40 COSTECH
Wananchi waunganisha nguvu Watoto wapate chakula shuleni
Homera ampongeza Rais Samia kwa ajenda ya nishati safi