November 12, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mwigulu mgeni rasmi kilele miaka 40 COSTECH

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 40 ya Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambayo kilele chake ni Novemba 17 mpaka 18 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 12, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema maadhimisho hayo yalizinduliwa mwezi Julai mwaka huu.

Amesema katika kipindi cha maadhimisho hayo kumefanyika shughuli mbalimbali, ikiwemo kliniki za ubunifu wakati wa maonesho ya Nanenane, maonesho ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika viunga vya Bunge.

“Shughuli nyingine ilikuwa ni tathmini ya utendaji wa Tume kwa muda wote wa kuwepo kwake na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 kwa kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu,” amesema Prof. Mkenda.

Aidha, amesema katika maonesho hayo kumebainika bunifu mbalimbali zikiwemo bidhaa zilizovuka kwenda sokoni.

Mfano, amesema mbunifu mmoja amegundua kifaa maalum cha Mkanda salama (postpartum belt) kinachomsaidia mama aliyejifungua kuzuia kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua.

Amesema mbunifu huyo ni miongoni mwa wabunifu walioshiriki maonesho ya viunga vya Bunge, na tayari amefungua kiwanda eneo la Kimara Suka Jijini Dar es Salaam.

“Tayari nchi za Ethiopia na Rwanda zimeonyesha nia ya kununua mikanda hiyo iliyogunduliwa na Mtanzania,” amesema.

Vile vile, amesema kuna mbunifu mwingine aliyegundua chanjo ya samaki na vifaranga, chanjo inayolenga kupunguza vifo vya samaki wanaofugwa majumbani.

Amesema chanjo hiyo tayari imetambuliwa na mamlaka za nje kwa ajili ya kuokoa samaki dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali.