May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mbarawa aelezea mafanikio ya TMA,kwa mwaka wa fedha 2023/24,


Na Penina Malundo, Timesmajira

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini(TMA )imeendelea na utoaji wa huduma , kudhibiti ,kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini,kutoa utabiri wa hali ya hewa, tafadhari za hali mbaya ya hewa pamoja na kupima na kufatilia mifumo ya hali ya hewa nchini.

Pia Serikali kupitia TMA imeendelea kutoa tabiri zake za kila siku,siku 10 na tabiri za muda mrefu ili kuhakikisha usalama wa watu na Mali zao ambapo usahihi wa utabiri kwa sasa umefikia asilimia 86 ambao ni juu ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Hadi sasa serikali kupitia TMA imekamilisja ufungaji wa rada za hali ya hewa katika Miko ya Kigoma na Mbeya na kufikisha jumla ya rada tano za hali ya hewa nchini.

Aidha wanatarajia utengenezaji mwingine wa rada mbili unaendelea katika kiwanda nchini Marekani ambapo zinatarajiwa kukamilika Novemba 2024.

Rada hizo zinatarajiwa kufungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma baada ya kukamilika kwake hivyo kukamilisha lengo la muda mrefu la kuwa na rada saba za hali ya hewa nchini.

Akielezea mafanikio ya TMA wakati akiwasilisha utekelezaji wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha unaoisha wa 2023/24,Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa anasema shughuli za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania zimeimarika katika mwaka wa fedha wa 2023/24, baada ya Serikali kuendelea kufanya uboreshaji wa utendaji wake.

Anasema kuna mafanikio mbalimbali TMA imeweza fanikiwa ndani ya bajeti hiyo ikiwemo Serikali imeingia mkataba wa kuboresha rada za hali ya hewa zilizofungwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza, ili kuendana na teknolojia ya kisasa ya rada za hali ya hewa.

Anasema , Serikali kupitia TMA imefanikiwa kukamilisha ufungaji wa mitambo mitano ya kutoa huduma za hali ya hewa katika viwanja vya ndege vya Songwe, Zanzibar, Arusha na Songea, ili kuboresha huduma hizo kwenye usafiri wa anga.

Anasema taratibu za ufungaji mitambo mitatu ya kupima hali ya hewa kwenye viwanja vya ndege vya Musoma, Iringa na Mpanda, zinaendelea.

Prof.Mbarawa anasema , Serikali imekamilisha ununuzi wa seti 28 za mitambo ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe ambayo imefungwa katika vituo vya hali ya hewa vilivyopo kwenye viwanja vya ndege vya Mtwara, Songea na Arusha, huku mitamboi mingine 25 inaendelea na maandalizi ya kufungwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Iringa, Njombe, Tanga, Dodoma, Singida na Kilimanjaro.

“Kuhusu kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kujenga uwezo kwa watumishi, Serikali kupitia TMA imeendelea na ujenzi wa jengo la ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 39,”anasema.

Anasema TMA inaendelea kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake na tabia ya nchi, ambapo tafiti nne zilichapishwa katika majarida ya kimataifa ya kisayansi yanaonesha matokeo mbalimbali.

“Miongoni mwa tafiti hizo ni kuhusu tathimini ya matukio ya hali mbaya ya hewa katika Bahari ya Hindi, tathimini ya ongezeko la joto kwa kipindi kati ya 1982 hadi 2022, tathimini ya hali ya mvua katika vituo vya hali ya hewa nchini na tathimini ya mabadiliko ya mvua na athari zake katika kilimo kwa nchi za Afrika Mashariki”anasema na kusisitiza.

“Mafanikio mengine TMA yamepata ni kutokana na umahiri wa mamlaka hiyo kwenye utoaji wa huduma za hali ya hewa, 2019 WMO iliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa kwa nchi zilizopo ukanda wa Ziwa Victoria.

“Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi. Sambamba na hilo, TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusini,” anasema Prof. Mbarawa.

Aidha Prof. Mbarawa anasema Serikali kupitia TMA imeendelea na utoaji wa huduma na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini kila siku, ambapo usahihi wa utabiri wake umeongezeka hadi kufikia asilimia 86 kiwango ambacho ni cha juu ya asilimia 70 ya kiwango kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Prof. Mbarawa anasema Januari 22 hadi 27, mwaka huu, TMA ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na kuendelea kukidhi voigezo vya kumiliki cheti cha ubora ((ISO 9001: 2015).

Akizungumzia utoaji wa huduma za hali ya hewa
Kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu,anasema kupitia ofisi zake tisa zilizopo katika bandari za Malindi – Unguja, Mkoani – Pemba, Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Ziwa Victoria katika Bandari ya Mwanza, Ziwa Tanganyika katika Bandari za Kigoma na Karema na Ziwa Nyasa katika Bandari ya Itungi na hivyo kuendelea kuchagiza shughuli za Uchumi wa Buluu.

Aidha, Prof.Mbarawa anasema wadau wa Uchumi wa Buluu ambao wameendelea kupatiwa huduma za hali ya hewa ni pamoja na watumiaji wa vyombo vya usafiri na usafirishaji, Watafiti na wachimbaji wa Mafuta na gesi, Mamlaka za bandari, Wavuvi, Wakulima wa mwani na matango bahari, wafugaji samaki na Vikundi vya usimamizi wa maeneo ya bahari na fukwe.

Anasisitiza kuwa kutokana na umahiri katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, mwaka 2019 Shirika la Hali ya Hewa Duniani liliichagua Tanzania kupitia TMA kuendesha kituo cha kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri wa hali mbaya ya hewa (Regional Specialized Meteorological Centre) kwa nchi zilizopo katika ukanda wa Ziwa Victoria.

“Kituo hicho kipo Dar es Salaam na kinahudumia nchi tano ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi,”anasema na kuongeza

” TMA iliteuliwa kutekeleza jukumu la kufuatilia ubora wa takwimu za hali ya hewa (data) zinazopimwa katika vituo vya hali ya hewa vya nchi sita (6) vya ukanda wa Afrika Mashariki ikujumuisha nchi ya Sudan Kusiniambapo majukumu haya TMA imeendelea kuyatekeleza kwa ufanisi na kuzidi kuitangaza nchi yetu kimataifa,”anasema.