June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Mapesa (MNMA) amewataka viongozi wa (MASO) 2025/26 kuwa viongozi bora

Na Rose Itono,Timesmajira

UONGOZI wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) umeitaka serikaliI mpya ya wanafunzi wa Chuo hicho (MASO) kuyatumia mafunzo elekezi yanayotolewa ili kuwa viongozi Bora

Akizungumza leo wakati akifungua mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo viongozi wa
serikali mpya ya wanafunzi kwa mwaka 2025/26 yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo hicho Kampasi ya Kivukoni Prof Mapesa ameitaka
Serikali mpya ya Wanafunzi wa Chuo (MASO), kuzingatia, kujifunza kwa weledi na kuyatumia mafunzo watakayoyapata katika semina elekezi ya kuwajengea uwezo ili wawe viongozi bora na wa kuigwa katika kipindi chote cha uongozi wao.

Prof. Mapesa amewataka viongozi kuyatumia mafunzo watakayoyapata kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuishi viapo vyao walivyoapa baada ya kuteuliwa kuongoza serikali ya wanafunzi wa chuo hicho.

“ Serikali ya wanafunzi (MASO) ni daraja kati ya wanafunzi na Menejimenti ya Chuo katika kuwasilisha maoni, kero, changamoto zinazowakabili wanafunzi hapa chuoni, hivyo mafunzo haya yatawajenga katika kutambua misingi ya sheria na taratibu za kufuata katika kuwasilisha mambo mbalimbali katika menejimenti”, amesisitiza Prof. Mapesa.

Pia ameitaka serikali ya wanafunzi kuwa mfano wa kuigwa kwa wenzao katika kuwashawishi kusoma kwa bidii ili kujiepusha na vitendo vya udanganyifu katika kipindi cha mitihani, kuwashawishi wanafunzi wenzao katika ulipaji wa ada pamoja na michango mbalimbali ya chuo, na kujiepusha na makundi ya migogoro katika muda wao ili waweze kuyafikia malengo ya kumaliza chuo kwa pamoja.

Amezitaja baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo kuwa ni pamoja na dhana ya Uongozi na Utawala Bora, Kanuni, Taratibu na Matumizi ya Fedha za Umma. Migogoro, Utatuzi, na Wajibu wa Serikali ya Wanafunzi.

Mada nyingine zitakazowasilishwa ni Uongozi Bora, Maadili, Haki na Wajibu wa Kiongozi Bora, Mawasiliano na Matumizi ya Muda, na Kazi za Dawati la Jinsia.

Semeni hiyo elekezi kwa Serikali mpya ya Wanafunzi ni maalumu katika kuwajengea uwezo viongozi wa serikali hiyo ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na weledi katika muda wote wa uongozi wao.