January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Makubi akutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Afya Korea

Na Mwandishi wetu,timesmajira, Online

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Taasisi ya kimataifa ya Afya-Korea (KOFIH) Prof. Chang Yup Kim.

Kikao hicho kimefanyika leo Julai 13, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo katika mazungumzo hayo wamekubaliana kushirikiana na Taasisi hiyo pamoja na kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kujadili na kutathmini maendeleo ya miradi yote inayofadhiliwa na KOFIH.

“Vikao hivyo vitasaidia kuona mapungufu yatakayo kuwepo na kuyarekebisha mapema kwa matokeo mazuri zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa hasa ya kuimarisha Afya nchini, katikab ngazi ya Afya ya msingi hadi ngazi ya rufaa na kupunguza au kumaliza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na Magonjwa ya kuambukiza.” Amesema Prof. Makubi

Kwa upande wake Kiongozi wa Taasisi ya kimataifa ya Afya-Korea (KOFIH) Prof. Chang Yup Kim amesema wataendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kufadhili miradi yenye thamani ya jumla Dola za Marekani Mil.5 sawa na Tsh: Bil 11,680,937,415.

“Fedha hizo ambazo zimetolewa kwa awamu ya pili zitaelekezwa kwenye miradi ya utolewaji wa huduma za Afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na uboreshaji wa huduma kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya jamii (NPHL).” Amesema Prof. Kim

Aidha, taasisi hiyo ya KOFIH inatarajia kufadhili takriban Dola za Marekani Mil. 12 sawa na Tsh. Bil. 28,034,273,797 kwa ajili ya mradi wa kuimarisha huduma za ufundi wa vifaa Tiba pamoja na elimu ya Afya kwa umma kuhusu Magonjwa yasiyoambukiza.

Kiongozi mkuu wa taasisi hiyo ya KOFIH ameishukuru na kuipongeza wizara ya Afya kwa kutoa ushirikiano mkubwa wakati wa utekelezaji na matumizi mazuri ya fedha za miradi iliyo chini ya KOFIH.