Na Allan Vicent, timesmajira, online Tabora
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba, amesema kama atachaguliwa kuingia Ikulu atahamasisha uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi.
Amebainisha hayo jana katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Town School ulioko katika Manispaa ya Tabora.
Amesema sekta ya kilimo ikisimamiwa ipasavyo wakulima hawatabaki kama walivyo sasa. Amebainisha kuwa kilimo chenye tija ndiyo mkombozi wa wakulima hapa nchini, hivyo kama atapata ridhaa ya kuwa Rais wa nchi hii Serikali yake itahamasisha wakulima na wadau mbalimbali kuwekeza katika sekta hiyo.
Profesa Lipumba ameongeza kuwa wakulima wakijengewa mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao na kuwatafutia masoko ya uhakika hakuna mkulima hata mmoja atakayeendelea kuwa maskini.
‘Uwekezaji katika sekta ya kilimo ni fursa muhimu sana itakayosaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuboresha shughuli za kilimo, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kubadilisha hali ya maisha ya wakulima hapa nchini,’ alibainisha.
Amefafanua kuwa yapo mazao mengi yanayostawi katika mkoa huo ikiwemo korosho hivyo kama yatapewa kipaumbele na kuhamasisha wadau kuwekeza katika mazao hayo nchi itapiga hatua kubwa sana katika uzalishaji.
Amesisitiza kuwa wakulima na wafugaji wakipewa elimu ya kutosha na pembejeo wanaweza kutafanya mambo makubwa sana, aliahidi kuwa kama watapata ridhaa watatenga asilimia 10 hadi 15 ya mapato ya serikali kwa ajili ya kuinua wakulima.
Aidha amebainisha kuwa wataboresha zaidi huduma za afya na elimu ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shule ili waweze kutimiza ndoto zao.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho upande wa Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, amesema kuwa kuboreshwa kwa huduma za afya kutapunguza kero wanazopata wajawazito katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha ili kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi wa umma, amesema kuwa chama hicho kikipewa fursa ya kuingia madarakani kitaboresha maslahi na kusimamia ipasavyo utendaji wao.
More Stories
TARURA Kilimanjaro yatimiza ahadi ya Rais Samia
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria
Wananchi wakubali yaishe Bangi kubaki historia Tarime