January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba

Prof. Lipumba asisitiza upimaji kuikabili Corona

Na Francis Peter

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameishauri Serikali kuendelea kuwapima watu wanaodhaniwa kuwa na Corona kwa lengo la kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo nchini.

Profesa Lipumba alitoa ushauri huo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisema ni muhimu kutilia mkazo upimaji wa wananchi wanaodhaniwa wana maambukizi na wasio na maambukizi hasa maeneo yanayopokea wageni kama kwenye miji ya Dar es Salaam na Arusha, Zanzibar na Mwanza.

Alisema ni muhimu sana kuwalinda madaktari na wauguzi wasiambukizwe virusi vya Corona kwa kuwapa vifaa vya kinga na mavazi maalum kwa wale wanaowahudumia wagonjwa.

“Maambukizi yakianza katika jamii ni hatari. Inakadiriwa katika kipindi cha siku tatu kila wenye virusi watano wanaambukiza watu wengine 11, kwa kasi hii ya maambukizi,ukiwa na walioambukizwa 100 hivi leo,baada ya siku 36 unaweza kuwa na walioambukizwa  1,285,500,”alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alisema jumuiya ya kimataifa imeanza kuzisaidia  nchi zingine kukabiliana na Corona akitolea mfano Ethiopia,Kenya na Congo (DRC) kuwa zimepata msaada wa Benki ya Dunia (WB) kukabiliana na maradhi hayo.

Aidha alisema serikali ioneshe shauku ya kutafuta misaada hiyo,  kwani Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) liko mbioni kukamilisha kutoa misaada ya dharura ya kukabiliana na athari za COVID -19 kwa nchi zaidi ya 90, huku kukiwa hakuna taarifa zinazoonesha kama Tanzania ina shauku yeyote ya kutafuta misaada hiyo.

Pia ameshauri Serikali kuimarisha usafi wa mazingira ya shule kuhakikiwa zinakuwa na vyoo vya kutosha, maji na sabuni ya kunawa kwenye vyoo na kabla mwanafunzi hajaingia darasani.

Profesa Lipumba alisema wakati huu ni wa tutumie changamoto ya Corona kujenga mfumo imara wa huduma za afya kuanzia vijijini na ngazi ya taifa.

Alishauri Serikali itenge fedha za kutosha kwenye sekta ya afya. “Kwa mfano mwaka wa fedha wa 2017/18 sekta ya afya ilitengewa sh. bilioni 712.2  sawa na asilimia 2.5 wakati Shirika

la Afya Duniani linapendekeza Serikali zitenge asilimia 15 ya bajeti kwa ajili ya sekta ya afya.

Alisema elimu kuhusu kuzuia maambukizi ni muhimu, hivyo tovuti ya Wizara ya Afya iwe na taarifa za kuzuia maambukizi ya maradhi  hayo na juhudi zinazochukuliwa na serikali kudhibiti maambukizi.

Profesa Lipumba alisema CUF inawataka Watanzania kuendelea kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii na kwamba wanamshukuru Rais John Magufuli kwa kutotangaza karantini.

Profesa Lipumba alisema katika nchi zingine palipo na maambukizi  watu wamezuiwa kutoka nje.

Katika hatua nyingine wanahabari mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuwa makini wakati wa kuandika habari zinazohusiana na ugonjwa wa hatari wa  Corona

 Ushauri huo umetolewa hivi karibuni mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na Afisa Afya Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Jonas Mcharo wakati wa mafunzo ya siku nne kuhusu ugonjwa huo.

“Katika kipindi hiki tumieni weledi wenu kuandika habari zinazohusiana na Covid-19, kila mtu anahitjai kupata taarifa kadiri zinavyoingia, hakikisheni mnatoa taarifa ambazo hazitaleta hofu ndani ya jamii”, alisema.

Pia aliwashauri wanahabari kuhakikisha wanapata taarifa sahihi zinazohusiana na ugonjwa huo kutoka vyanzo sahihi vilivyoelekezwa na Serikali.

“Tayari Serikali ishatoa taarifa zinazohusiana na Corona zitakavyokuwa zikitolewa, fuateni agizo hilo ili kupata taarifa za uhakika na za kweli”, alisema.

Aidha alitoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kutoa taarifa zinazohusiana na ugonjwa huo haswa kwa wageni wanaoingia maeneo yao kutoka nje ya nchi.

“Pale itakapobainika kuna mtu ameingia nchini, tafadhali toeni taarifa ili taratibu zilizowekwa kuhusiana na wanaoingia nchini zifuatwe; lengo la Serikali ni jema katika kupunguza na kuzuia maambukizi hapa nchini”, alisema.

Aliongeza, “Hata kama ni jamaa yako, mshauri ya kuwa kuna utaratibu uliowekwa na Serikali ikiwemo kupima na kukaa karantini, kwa njia tutazuia maambukizi haswa toka wka wale wanaoingia nchini kutoka nchi zilizoathirika zaidi”.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha maofisa wa afya kutoka wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, wale wa ngazi ya Mkoa pamoja na wanahabari wa mkoa wa Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuwajengea washiriki pamoja na mambo mengine uelewa kuhusu ugonjwa huo.