May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Lipumba apuliza kipenga cha uchaguzi CUF

Na Hadija Bagasha Tanga,

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewataka wanachama wake wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi Mkuu ujao kuanza maandalizi mapema ikiwemo kutangaza nia.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akizungumza na Majira mkoani hapa jana.

Profesa Lipumba aliwataka wenye uthubutu wa kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais wasione hofu kuwania nafasi hizo, bali waanze maandalizi mapema ili pale kipenga kikipigwa wawe wapo tayari.

“Nafasi za siasa zinahitaji maandalizi hivyo niwatake wanachama wangu wenye nia ya kuwatumikia wananchi wa nchi hii waanze kujitayarisha kwa ajili ya kugombea,”alisisitiza Profesa Lipumba.

Aidha amesema suala la kutangaza ni tafsiri yake ni kuchukua fomu,kujaza na kurejesha kisha kusubiri mchujo wa kura za maoni ambapo suala hilo haliwezi kuathiriwa na uwepo wa ugonjwa wa Corona.

Vile vile aliwahamasisha wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwa ajili ya kuwatumikia wananchi badala ya kurudi nyuma kwa kuhofia uwezo wao.

“Wanawake ni miongoni mwa viongozi bora, lakini kinachowashinda ni uwoga wao lakini niwatake watumie mafanikio ya wanawake wenzao waliothubutu kama chachu ya wao nao kugombea,”amesema Prof. Lipumba na kuongeza;

“Ninavyoona mimi changamoto iliyokuwepo ni kuitisha vikao vya kura za maoni katika kipindi hiki cha uwepo wa ugonjwa wa covid19 kwani wataalamu wa afya wametushauri kuepuka mikusanyiko.”

Aidha Prof. Lipumba amesema watahakikisha wanasimamia sera ya Chama hicho ya haki sawa na furaha kwa wote . Hata hivyo akizungumza athari za ugonjwa wa corona katika shughuli za kichama amesema kuwa zimezuia shughuli za uimarishaji Chama katika ngazi za wilaya,Majimbo na Kata .