December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Lipumba aichambua bajeti

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online

SERIKALI imeshauriwa ipitie upya mpango wa tatu wa maendeleo ili ujikite katika kuleta mapinduzi ya kilimo na hatimaye yachochee mapinduzi ya viwanda.

Awali akiichambua bajeti ya Serikali, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni bingwa wa uchumi duniani Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa, bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 ni ya kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Profesa Lipumba amesema kuwa, bajeti hiyo itajielekeza katika utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa katika maeneo matano ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Profesa Lipumba amesema kuwa, pungufu kubwa la mpango wa tatu ni kukwepa uhalisia kuwa Tanzania haijafanikiwa kuasisi mapinduzi ya kilimo ambayo ndiyo msingi wa kuleta mapinduzi ya viwanda.

“Malengo ya Mpango ni kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, hata hivyo hotuba ya bajeti imejiwekea lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 5.6 mwaka 2021 na kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.2 ifikapo mwaka 2023,

“Ni wazi lengo la kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia nane haliwezi kufikiwa,”amesema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba amesema, ili wabunge wajadili vizuri bajeti wanahitaji kuwa na kitabu kinachochambua maendeleo ya uchumi ya sekta zote ikiwemo kilimo,viwanda, madini, ujenzi, miundombinu, afya, elimu, ajira, mfumko wa bei, fedha na mabenki, mgawanyo wa bajeti katika sekta mbalimbali lakini wabunge wamepewa kitabu cha hali ya uchumi wa Taifa Juni 10, 2021 baada ya kujadili na kupitisha bajeti za sekta zote.