Na Esther Macha Timesmajira Online, Mbeya
KATIBU Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kukuza maendeleo ya Sekta ya Maji hivyo itaendelea kupitia sera na taratibu mbalimbali ili kuhakikisha mazingira ya ushirikiano yanaendelea kuimarika.
Prof. Katundu amesema hayo wakati wa kongamano la wadau wa Sekta ya Maji la Mwaka 2023 jijini Mbeya.
Amesema serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ikilenga kuhakikisha kila Mtanzania anafikiwa na huduma ya maji na kwamba mafanikio yote yaliyofikiwa katika lengo hilo ni makubwa na yote yamefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri wa Serikali na sekta binafsi.
“Nichukue nafasi hii kuwahakikishia sekta binafsi kuwa serikali inatambua mchango wenu na inaendelea kuchambua mahitaji yenu na iko tayari kushirikiana nanyi na hata kuwasaidia pale ambapo mtakakuwa mnahitaji msaada” Professa Katundu amesema.
Amewataka wadau hao wa Sekta ya Maji kujadiliana katika kongamano hilo ili kupata muongozo na utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli za wadau wa maji ili kuimarisha ushirikiano.
Aidha, amewaagiza watendaji wa Wizara ya Maji kuwasilisha rasimu ya Sera inayoendelea kufanyiwa maboresho kwenye uongozi wa Jumuiya ya Wasambazaji wa Maji nchini (ATAWAS) ili watoe maoni na mchango wao katika kuiboresha.
Kongamano la wadau wa sekta ya maji linafanyika kwa siku tatu jijini Mbeya na limeandaliwa na Jumuia ya wasambazaji wa maji nchini (ATAWAS) likiwa na kaulimbiu isemayo “PPP for Sustainable Water and Sanitation Services ”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi