April 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPRA,Generation Samia kutangaza fursa za zabuni kwa makundi maalumu Mwanza

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Licha ya uwepo wa sheria ya kuzitaka taasisi nunuzi kutenga asilimia 30 ya mpango wao wa bajeti  kwa ajili ya makundi maalumu,bado makundi hayo hayajitokezi kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kupata zabuni hizo.

Hivyo kutokana na changamoto hiyo Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma(PPRA) kwa kushirikiana na Generation Samia,wameanda kongamano la wazi la fursa za uchumi ambalo linabeba ujumbe  usemao mgao wa asilimia 30 za Samia kupitia mfumo wa NeST,litakalofanyika Machi 29,2025 Kwa Tunza wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari  mkoani hapa Machi 26,2025,Meneja wa Huduma za Kanda Ofisi ya PPRA Kanda ya Ziwa Juma Mkobya,amesema lengo la kongamano la mgao wa asilimia 30 za Samia kupitia mfumo wa NeST ni kusaidia vikundi ambayo vipo na kama havipo wananchi wajiunge na kusajiliwa katika  Halmashauri zao kisha wasajiliwe  kwenye mfumo wa NeST ili waweze kupata hizo fursa.

Mkobya, amesema ni agizo na maelekezo kwa taasisi yoyote ile hata kama ni PPRA yenyewe ina zabuni zake mfano za bilioni 5, ofisi ya Mkoa kupitia ofisi ya Katibu Tawala Mkoa(RAS), wameandaa mpango wao  wa ununuzi wa mwaka 2024/25 labda zabuni za bilioni 200 asilimia 30 ya hiyo thamani lazima watoe kwa makundi maalumu.

“Shida tunayopata,kwa mwaka fedha hizo zinatengwa  zinaishia hewani kwa sababu hakuna makundi maalumu ambayo yanajitokeza kuomba kazi ambazo wametengewa fedha.Na mpaka sasa  jumla ya makundi maalumu 550 yamesajili katika mfumo wa NeST,na zabuni zenye thamani ya zaidi ya bilioni 15, zimeishatolewa kwenye hayo  na kwa Kanda ya Ziwa makundi maalumu ambayo yamesajili katika mfumo wa NeST ni zaidi ya 70,”amesema Mkobya.

Kwa upande wake Msemaji wa Generation Samia na Balozi wa Mfumo wa NeST,Sonnatah Nduka, amesema wametambua kuwa Serikali inatumia zaidi ya asimilia 70 ya bajeti yake kwenye masuala ya ununuzi wa umma.

Hivyo wamelitazama jambo hilo kama fursa ambayo wanapaswa kupeleka kwa Watanzania,kupitia ununuzi wa umma katika kutekeleza miradi mbalimbali na mambo mengine ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu ambapo  Serikali unanunua huduma,bidhaa na kazi za ujenzi hivyo utekelezaji hayo kwa  kutoa zabuni kwa wananchi wenye sifa.

Sonnatah, amesema kwa kuzingatia hayo Generation Samia,kwa Mkoa wa Mwanza wamezimulika fursa za zabuni za Serikali zilizopo na wametuambia imeweka mfumo wa NeST,ambao unatumika kutoa zabuni hizo kwa uwazi na usawa.

Amesema,kupitia mfumo wa NeST,makundi maalumu ya vijana,wazee, wanawake na wenye ulemavu,yameisha pata mgao wa zabuni zenye thamani ya takribani bilioni 15 huku akisisitiza kuwa kwa Mkoa wa  Mwanza kuna fursa nyingi katika sekta hiyo ya ununuzi wa umma ambazo zipo hadi ngazi ya Serikali za Mitaa.

“Lakini wananchi wengi hawafahamu fursa hizo ambazo zipo za ujenzi,usafi,lakini pia Serikali inahitaji huduma,kununua bidhaa, na kadhalika,sisi kazi yetu Generation Samia jukwaa la fursa ni kufungua “code”, za fursa mkoani Mwanza  kwa kushirikiana na PPRA na wadau wengine,” amesema Sonnatah na kuongeza kuwa:

“Kuna makundi 500 ambayo yamejiunga na mfumo wa NeST na wananchi tupo zaidi ya milioni 64, maana yake taarifa zaidi zinatakiwa kwenda kwa wananchi ili tuweze kufikia lengo la kila Mtanzania kushiriki katika keki hii ya taifa, ambapo asilimia 70 ya bajeti ya Serikali ipo kwenye manunuzi ya umma,na sisi  tunaenda kuisemea ili watu wajue,waione hiyo fursa na waweze kunitumia kupitia kongamano hilo,”.

Hata hivyo amesema,wanaamini baada ya kongamano hilo Watanzania wengi zaidi watajisajili kwenye mfumo wa NeST na idadi ya vikundi vya wanawake,vijana,watu wenye ulemavu na wazee vinavyopata zabuni za Serikali  kupitia mfumo wa NeST wa mgao wa asilimia 30 za Samia vitaongezeka.