Na Mwandishi wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefungua Ofisi katika kanda tano nchini na kuwa na jumla ya kanda sita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika kusimamia sekta ya ununuzi wa umma.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Eliakim Maswi katika kikao cha wafanyakazi wa Mamlaka kilichohudhuriwa na Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) ngazi ya Mkoa, kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Amezitaja ofisi hizo za Kanda kuwa ni Kanda ya Ziwa (Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza), Kanda ya Kati (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora), Kanda ya Kaskazini (Jengo la PSSSF jijini Arusha), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Jengo la NHIF jijini Mbeya) na Kanda ya Kusini (Jengo la PSSSF mjini Mtwara). Orodha hiyo inafanya Mamlaka kuwa na jumla ya ofisi sita za kanda kwa kujumlisha na ofisi ya kanda ya Pwani iliyopo jengo la Wizara ya Fedha Jijini Dar es salaam iliyokuwepo awali.
‘’Naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka kusogeza huduma kwa wananchi. Hii ni sehemu ya mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wake. Sasa wananchi hawatakuwa na ulazima wa kuja Dodoma ili wafike PPRA, kila kanda watahudumiwa kikamilifu,” amesema Bw. Maswi.
Ameongeza kuwa kila Kanda imewezeshwa kuwa na wafanyakazi wa idara zote ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wananchi na wadau wa sekta ya ununuzi katika maeneo yao, akisisitiza kuwa wameweka nguvu pia kwenye utoaji wa huduma za Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST).
Aidha, amewasihi wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuendelae kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia uzalendo ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana kwenye ununuzi wa umma.
“Ninawaomba watumishi wenzangu mwende mkatengeneze uhusiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka, hii itawasaidia kuendelea kuaminika kwa wananchi na mtapata ushirikiano mkubwa kwa viongozi wa mikoa hiyo,” amesisitiza.
Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Bw. Maulid Kipeneku ametoa rai kwa wafanyakazi PPRA kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia sheria na taratibu. Aliwapongeza wafanyakazi hao kwa jinsi wanavyotoa huduma kwa wananchi, na kwamba anaamini wafanyakazi hodari watapatikana ndani ya Mamlaka hiyo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua