November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PPAA yashiriki kongamano la 16 la ununuzi wa umma Afrika Mashariki

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeshiriki katika Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha. Kongamano hilo lilianza tarehe 9 – 12 Septemba 2024.

Aidha, katika kongamano hilo, PPAA imeshiriki pia kufanya maonesho ya kutoa elimu kuhusu majukumu, malengo na mafanikio yake kwa umma na wadau wa sekta ya ununuzi.

Kongamano hilo la siku nne (4) limewakutanisha wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo ni mwenyeji Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepata fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu katika sekta ya ununuzi wa umma katika ukanda huo.

Taasisi zinazosimamia sekta ya ununuzi wa umma nchini zimepata fursa ya kunadi huduma zake na fursa mbalimbali zinazotolewa. Taasisi hizo ni Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) pamoja na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).

Kongamano hilo limewakutanisha wadau wa ununuzi zaidi ya 1,000 limeongozwa na Kaulimbi: “Digitalization for Sustainable Public Procurement” (Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu).