November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi,Sungusungu waungana kukomesha uhalifu

Na Lubango Mleka, TmiesMajira Online Igunga.

JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na Jeshi la Jadi (Sungusungu), wameungana kukomesha matukio ya kiuhalifu yaliyoibuka kwa baadhi ya Kata na na kusababisha wananchi wa Kata ya Ibologero kukumbwa na taharuki,sintofahamu juu ya usalama wao na mali zao.

Ofisa wa Polisi Eddah John kutoka kitengo cha Ushirikishwaji wa Jamii ndani ya Jeshi la hilo wilaya ya Igunga akitoa elimu ya Polisi jamii kwa wakazi wa Kata ya Ibologero ambapo zaidi ya 3000 waliojitokeza katika mkutano wa hadhara hivi karibuni.

Ambapo majeshi hayo yalikazimika kuitisha mkutano wa hadhara katika kata hiyo ya Ibologero kwa lengo la kuwatambua wahalifu na kutoa elimu juu ya mipaka ya kazi, mauaji ya kikatili, ramli chonganishi, ukatili wa kijinsia, usomwaji wa mapato na matumizi, utoaji wa taarifa na ushahidi katika vyombo vya kisheria ambapo zaidi ya wananchi 3000 walihudhuria mkutano.

Mtemi wa Sungusungu Wilaya ya Igunga Kalenji Masano,akizungumza katika mkutano huo ametoa pole kwa wananchi wa kata hiyo kufuatia kukumbwa na matukio ya wizi uliotokea jana usiku na hivi karibuni.

“Sikuwa na ratiba ya kuja hapa ila imenilazimu kuja kuungana nanyi kutafutia ufumbuzi tatizo hili la wizi lililo wakumba,ninaomba mnisikilize kwa makini sana ntakapo toa nasaha na elimu niliyotumwa na viongozi wangu kuanzia ngazi ya mkoa mpaka wilaya,”amesema mtemi Masano.

Mtemi wa Sungusungu Wilaya ya Igunga mkoani Tabora Kalenji Masano akitoa elimu juu ya Ulinzi wa Jeshi la Jadi (Sungusungu) akitoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Ibologero hawapo pichani.

Amesema kuwa,anatoa elimu juu ya Sungusungu na Serikali,ikiwemo suala la mipaka ya kazi kati ya Sungusungu, Jeshi la Polisi,viongozi wa vijiji na Kata kwani hapo nyuma Sungusungu walikuwa wanakosana na Polisi kwa sababu ya kutokujua majukumu yao na mipaka ya kazi.

“Ulikuwa ukimuona polisi ni mbio unajua anakuja kukukamta, lakini baada ya maboresho ya jeshi letu la Sungusungu leo tunatembea na askari Polisi na tunafanya kazi pamoja,” ameseema Mtemi Masano.

Kwa Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Jamii Polisi Wilaya ya Igunga, Eddah John amepongeza Jeshi hilo la jadi la Sungusungu kwa kazi nzuri wanayoifanya kuzuia na kukamata wahalifu.

“Jeshi la Sungusungu ni Jeshi ambalo linajitoa sana katika kulinda na kuzuia uhalifu katika maeneo yetu, niliwaita na kutaka kujua wanafanyaje kazi zao walikuja na nikawatambua na kuwapatia mafunzo ili wasije kwenda kinyume na sheria, na ndio maana hata leo nimekaa na nimesikiliza nini kamanda na Mtemi wa Sungusungu watasema, ili kama anakwenda kinyume na sheria basi mimi nianze naye, nashukuru amesema yote ambayo ni matakwa ya kisheria,” amesema John.

Pia amesema kuwa, Ibologero ni sehemu ya kivutio cha uwekezaji, hivyo kama wanataka kuendelea kuwa kivutio cha uwekezaji haiwezekani wakaruhusu uhalifu utokee katika eneo hilo.

“Kama tukiruhusu uhalifu utatokea basi hatutopata wawekezaji,watahamisha biashara zao na eneo hili litaathirika kiuchumi, ila kama mtataka kuendelea na uhalifu mtakuwa mmetualika tuje tupige kambi hapa na mkitushinda tutaalika na majeshi mengine na mtakuwa mnalala saa 12 jioni hakuna kutoka mimi nawaambia mnavyotualika tutakuja kweli,” amesema John.

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo akiwemo Mussa Zephania,wamelipongeza Jeshi la Sungusungu na Polisi kwa kuwapatia elimu juu ya ulinzi katika maeneo yao na wameahidi kushirikiana nao ili kukomesha uhalifu na wizi ambao umeibuka katika kata yao.

“Mimi ninawaomba viongozi watusaidie kuimarisha usalama wa eneo letu la Ibologero na pia wananchi tujitoe kulinda na kushirikiana na majeshi yetu katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu,”amesema Zephania.

Huku Asha Shabani,amesema kutokana na elimu hiyo wameahidi kushirikiana na majeshi hayo katika kukomesha uhalifu, wahalifu na wafadhili wao kwa kutoa taarifa za siri kwa Jeshi la Polisi na ikiwa wataitajika kutoa ushahidi mahakamani.