January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rpc Muroto akionyesha silaha zilizokamatwa

Polisi yatahadharisha wapambe wagombea urais mikutano ya CCM

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama limejipanga kudhibiti vitendo vya utapeli kwa washiriki uchaguzi kwa kujifanya wapo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (SAC), Gilles Muroto amesema wamejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili mkutano huo ufanyike kwa usalama na amani bila vitendo vya utapeli kutamalaki.

“Jeshi limejipanga kuhakikisha yeyote atakayejaribu kufanya utapeli wa kujifanya yupo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa hawataondoka Dodoma, wajipange kubakia ili kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” alisema Muroto.

Katika Mkutano Mkuu wa CCM ulioanza leo Julai 7 hadi 12, mwaka huu, utachagua na kupitisha wagombea wa nafasi ya Rais Tanzania Bara na Zanzibar kwa tiketi ya CCM.

Muroto amesisitiza; “Sitataka kuona vitendo vya utapeli katika mkutano huu unahudhuriwa na viongozi wakuu wa kitaifa, viongozi wa Serikali wastaafu, viongozi wa vyama rafiki wa CCM kutoka mataifa mbalimbali duniani na kutoka katika mikoa mbalimbali.”

Muroto amesema mkutano huo unaotarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 3,000 hatapenda kuwaona watu wanaotaka kutenda vitendo vya kitapeli  kwa kujifanya wapo karibu na viongozi.

Amesema uzoefu unaonesha kwamba katika mikutano kama hiyo wamekuwa wakihudhuria watu mbalimbali wakiwemo wapambe wa wagombea, familia za wagombea, wapiga debe, wajasiliamari, lakini pia wanakuwepo watu wabaya ambao wanatumia fursa hiyo kutekeleza azma yao ya kitapeli.

Muroto amesema makundi hayo ambayo yanapanga kufanya vitendo vya kihalifu yasije yakaingia katika mtego ambao hawakutarajia, jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kulinda vitendo hivyo vya kitapeli visitokee.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limefanya oporesheni za kuwasaka wezi wa magari na kufanikiwa kukamata watuhumiwa wawili ambao wamekiri kufanya matukio mbalimbali ya wizi na unyang’anyi wa magari nchini na ya kutoka nje sambamba na kuwapa dawa ya kulevya abiria katika mabasi kupitia biskuti.

Pia katika oporesheni hiyo wamekamata silaha mbili aina ya bastola na risasi 14 inayomilikiwa na Jumbe Kamugisha (46). Kamugisha ni mkazi wa Chanika Msongola  Jijini Dar es Salaam. Pia Polisi walikamata vidonge 124 aina ya Rolvan na paketi moja ya biskuti wanazotumia wahalifu kulewesha abiria kwenye mabasi.

Silaha nyingine iliyokamatwa ni aina ya browning pamoja na risasi 15 inayomilikiwa na George Semtego (36) Mbondei, mfanyabiashara, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam. Muroto amesema silaha hizo zinamilikiwa kihahali lakini zimekuwa zinatumika katika matukio ya kihalifu.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa hawazilipii lakini pia hazikuhakikiwa na kupewa namba za silaha za nchini.