Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza, limewatahadharisha viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wao kuzingatia sheria, kanuni, na maadili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani, utulivu, na usalama.
Pia, jeshi hilo la polisi limejipanga vyema kwa rasilimali na vifaa kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani na kuwachukulia hatua za kisheria,watu au vikundi vya wanasiasa vitakavyojaribu kuwatisha na kuwazuia wananchi waliojiandikisha kupiga kura, ili kutimiza wajibu na haki yao ya kikatiba, au kupora vifaa vya uchaguzi.
Kauli hiyo ilitolewa Novemba 23,2024, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Willbrod Mutafungwa, katika mkutano na wadau wa uchaguzi uliofanyika katika uwanja wa Polisi Mabatini, wilayani Nyamagana, ambapo walishirikishwa viongozi wa dini, vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi, na makundi mbalimbali ya kijamii.
“Polisi tunalo jukumu la ulinzi na usalama, kuhakikisha kwamba sheria inazingatiwa ili kuwe na utulivu, usalama, na amani. Sote tuone umuhimu huo ili uchaguzi upite salama. Naamini lazima hayo yafanyike ili watu wapate nafasi ya kutimiza wajibu wao na haki yao ya kikatiba, na wanaofikiria kupora vifaa vya uchaguzi wafikirie tena,” amesema Mutafungwa.
Ameongeza kuwa, ingawa jeshi hilo lina majukumu mengine, linawajibika kusimamia uchaguzi katika maeneo mahsusi, lakini haliondoi jukumu lake la ulinzi wa raia na mali zao ili watu waweze kufanya kazi zao za maendeleo kwa usalama.
Mutafungwa amesema, polisi wataendelea kusimamia mikutano ya kampeni ili kulinda usalama wa wananchi na kuhakikisha kwamba mikutano hiyo inafanyika kwa usalama na utulivu. Alisisitiza kuwa sheria zitatekelezwa na kwamba watachukua hatua kali dhidi ya watu wanaojaribu kuvuruga uchaguzi, bila kuonea mtu huruma.
“Kazi ya polisi ni kutoa ulinzi kwa viongozi na watendaji wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wakiwemo wa vyama vya siasa na wafuasi wao bila kujali itikadi yoyote. Wasimamizi wa uchaguzi wasihofu, kwa sababu tumejipanga kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani na kushirikiana na kila mtu,” alisema.
Kamanda Mutafungwa amesema mchakato wa kupiga kura hadi kutangaza matokeo utakuwa huru na utulivu utakuwepo kuanzia sasa hadi hadi siku hiyo na baada ya uchaguzi usalama utaendelea kuwepo mkoani Mwanza.
Amewataka wadau wa uchaguzi kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na kuzingatia sheria, akisisitiza kwamba viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri amani kanisani na misikitini ili watu watimize wajibu wao.
Pia,amewataka wananchi kujiepusha na mikusanyiko isiyo halali wakati wa uchaguzi, kwani ni jukumu la polisi kudhibiti mikusanyiko hiyo na kuisimamisha.Wananchi wasijichanganye na vikundi vinavyoweza kuleta vurugu, kwani mikusanyiko hiyo itadhibitiwa na polisi.
Mutafungwa alionya kuwa kuchelewa kutangaza matokeo ya uchaguzi kunaweza kusababisha watu kupoteza imani, na kujiunga katika vikundi vitakavyozalisha vurugu.Amesema baadhi ya vyama vimekuwa vikikataa matokeo licha ya kuwa na mawakala wao katika vituo vya kupigia kura.
“Maandamano haramu hatutaruhusu wala kuvumilia. Tumejipanga kuyadhibiti, na wale watakaojaribu kuhamasisha maandamano hayo yawepo wasithubutu. Wananchi wajitokeze kupiga kura bila hofu, na vyama vya siasa vifuate miongozo iliyopo na inayosimamiwa na polisi,” aliongeza.
Mwenyekiti wa CHAWATA Wilaya ya Kwimba, Julius Musa,ameaema walemavu wanahitaji uchaguzi wa amani, kwani hawana pa kwenda ikiwa vurugu zitatokea.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua