Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
JESHI la Polisi jijini Mwanza linamsikilia mtuhumiwa anayefahamika kwa jina la Hamisi Omary mwenye umri wa miaka 19 mkazi wa Nyasaka Msumbiji kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Katunguru ambaye pia ni mkazi wa mtaa wa Msumbiji Kata ya Kawekamo Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.
Inadaiwa kuwa , tukio hilo limetokea Desemba Mosi mwaka 2020, saa 5 asubuhi katika mtaa wa Msumbiji Kata ya Kawekamo wilayani Ilemela ambapo mwanafunzi huyo alikutwa ameuwawa katika chumba alichokua anaishi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne amesema, mwanafunzi huyo aliyefahamika kwa jina la Vicent Renatus anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 17 ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo na mkazi wa mtaa huo, alikutwa ameuwawa katika chumba alichokua akiishi huku mwili wake ukiwa na majeraha shingoni na chumbani kwake kukiwa kumeibiwa vitu mbalimbali vya nyumbani ikiwemo runinga(television) na radio(SUB WOOFER).
Amesema, jeshi hilo baada ya kupata taarifa hizo lilifanya msako mkali ulioongozwa na taarifa za kiintelijensia na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.
Baada ya kuhojiwa kwa kina, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji ya mwanafunzi huyo na aliwaonesha askari vitu vilivyopora kwa marehemu na kwenda kuviuza kwa Erasto Jackson mwenye miaka 22 mkazi wa Kitangiri.
Jeshi hilo pia lilimkamata na kuhojiwa mnunuzi huyo kwa tuhuma za uhalifu sugu wa kupokea mali za wizi na kwa sasa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wengine wa tukio hilo.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â