January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi waanza operesheni wanaopita njia za DART

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Dar

WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani, wameanza operesheni maalum ya kukamata wanaopita kwenye barabara za mabasi hayo wakiwemo waendesha bodaboda, bajaji, magari binafsi, magari ya serikali na yale ya majeshi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa zoezi la ukamataji wa madereva wanaopita kwenye barabara za mabasi hayo eneo la Kinondoni Mwanamboka, mkoani Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dumu Mwalugenge kutoka Makao Makuu ya Trafiki, amesema zoezi hilo ni endelevu.

Amesema linalenga kukomesha vitendo vya uvunjifu wa sheria vinavyofanywa na baadhi ya wananachi wasiotaka kutii sheria bila shuruti.

“Unaona baadhi ya madereva wa pikipiki wakiwa wamekamatwa, hii ni kuonesha msisitizo kwamba lazima sheria zifuatwe na kusiwe na ulazima wa kutumia nguvu mara kwa mara, kwani jamii iliyostaarabika inafuata sheria kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuzuia ajali za mara kwa mara zinazoendelea kujitokeza kwenye barabara za mabasi hayo.

Mkaguzi Mwalugenge amesema barabara hizo zimejengwa mahsusi kwa ajili ya mabasi ndio maana hata ukiziangalia vizuri michoro yake chini kwenye sakafu za barabara imendikwa “Bus” hivyo ni pekee kwa ajili ya mabasi na sio bodaboda, bajaji wala magari binafsi na hata ya Serikali.

Aidha amesema madereva wa magari ya Serikali ndio wanaongoza kwa kuvunja sheria hasa kupitisha magari kwenye barabara za mabasi hayo, hivyo akatoa wito kwa wale wenye tabia hiyo kuacha mara moja.

“Madereva wa Serikali hawako juu ya sheria natoa onyo waendelee kutii sheria bila shuruti ndiomaana unaona operesheni hii inayoambatana na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara za Mabasi Yaendayo Haraka inaendelea” amesema.

Hivi karibuni ajali nyingi zimetokea kwenye mfumo wa barabara za mabasi hayo zikihusisha pikipiki, na magari binafsi jambo ambalo linaongeza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara hizo, lakini pia kwa waenda kwa miguu.