January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi Shinyanga yakamata watuhumiwa 231 kwa makosa tofauti

Na Suleiman Abeid, TimesMajira,Online Shinyanga

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limewakamata watu 231 wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha, wakata mapanga na waganga wa jadi wanaojihusisha na vitendo vya upigaji ramli chonganishi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Devota Magiligimba amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia opresheni maalumu ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu na kuzuia makosa mbalimbali ndani ya kipindi cha Januari, 2021 hadi Aprili 25 mwaka huu.

Kamanda Magiligimba alisema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa 169 tayari wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria na watuhumiwa wengine 62 waliobaki watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kuhusiana na makosa yao kukamilika.

Miongoni mwa vitu vilivyokamatwa katika Opresheni hiyo ni bunduki 14 ambazo 13 ni magobore na Shotgun moja ambayo imetengenezwa kienyeji, bangi kiasi cha kilo 65, mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari sita, madawa ya kulevya aina ya Heroine gramu 300.

Vingine ni mirungi kilo tatu na gramu 250, magari mawili ambayo ni Toyota Sprinter yenye namba za usajili T.673 AYK na Toyota IS namba T.377 DNA, Pikipiki 19 aina ya SANLG, mazao ya misitu mbao vipande 711, pombe haramu aina ya gongo lita 407 ikiwa pamoja na mitambo minne ya kutengenezea pombe hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga, Devota Magiligimba akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na watuhumiwa zaidi ya 200 waliokamatwa mkoani humo wakituhumiwa kwa vitendo mbalimbali vya uhalifu ikiwemo upigaji ramli chonganishi. (Picha na Suleiman Abeid)

“Lakini pia tumefanikiwa kukamata boksi 30 za kondomu zilizopigwa marufuku, TV 14, Radio Sabufa sita, mabati 15, betri za magari 12 na za pikipiki sita, betri za solar saba, mafuta ya dizeli lita 240, Engine oil lita 120, vitenge vipande 42 pamoja na magauni 15 ya vitenge, nondo 36 ikiwemo bidhaa mbalimbali zilizokwisha muda wake wa matumizi,”

“Vitu vingine tulivyokamata ni pamoja na vifaa tiba, mapanga yanayotumika kwenye kufanyia vitendo vya uhalifu, mifuko ya nailoni iliyopigwa marufuku 1,200 na mawe yanayohisiwa kuwa na dhahabu gramu mbili,” ameeleza.

Kamanda huyo amefafanua kuwa miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa watuhumiwa 71 ni wanawake wanaojishughulisha na shughuli za uganga wa jadi ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya kupiga ramli chonganishi.

“Misako hii ni endelevu ili kubaini mitandao yote ya kiuhalifu na kukabiliana nayo, nitoe wito kwa wananchi wetu waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi letu ili tuweze kukomesha vitendo vya uhalifu katika mkoa wetu, na tutaendelea kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivi,” ameeleza Magiligimba.