*Wananchi watahadharishwa juu ya imani potofu
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewataka wananchi kuachana na imani potofu ikiwemo kuamini katika ushirikina ambao unaweza kuchochea mauaji, ukatili na matukio mengine ya jinai katika baadhi ya maeneo, hususani Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 17, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP.Wilbrod Mutafungwa,wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Bwisya wilayani humo kwa lengo la kutoa elimu ya usalama na kuhimiza utunzaji wa amani.

DCP.Mutafungwa amesema jukumu la kudumisha amani ni la kila mmoja, hivyo kila mmoja anapaswa kushiriki kikamilifu kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na watu wanaojiita wataalamu wa kusaka wachawi maarufu kama ‘Kamchape’.
Amesema kundi hilo limekuwa likijihusisha na uporaji wa mali, utapeli kwa kutumia ramli chonganishi na kuingia katika nyumba za watu kwa madai ya kuondoa ushirikina jambo ambalo linajenga chuki na kukiuka sheria za nchi.
“Hatutaruhusu watu binafsi au viongozi kuwatapeli wananchi kwa kisingizio cha matambiko au imani za kishirikina. Jeshi la Polisi liko tayari kulinda raia na mali zao wakati wote,” amesema DCP. Mutafungwa.
Sanjari na hayo ametoa wito kwa wananchi kuacha kuwahifadhi wahalifu hao (Kamchape)badala yake watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili hatua zichukuliwe dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Aidha amesema watu 21 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na vitendo hivyo vya kihalifu na uchunguzi dhidi yao unaendelea, utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kisiwa cha Ukara, akiwemo Maritha Nyangeta na Samsoni Ibrahim,
wamesema wamekuwa wakilengwa na kundi la Kamchape linalopita nyumba kwa nyumba, kuwatisha na kuwanyang’anya mali zao kwa madai ya kuwatoa uchawi, hali iliyozua taharuki na kuathiri maisha yao ya kila siku.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi