December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi kutumia R4 za Samia kulinda wananchi, mali zao

Na Yusuph Mussa, Timesmajiraonline, Lushoto

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Jeshi la Polisi nchini litaendelea kuwalinda wananchi na mali zao na ili kufikia azma hiyo, litatumia R4 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambazo zitawafanya kufanya kazi zao kwa weledi.

Amesema Rais Dkt. Samia amekuja na falsafa za mambo manne ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya, ambapo kama itafuatwa falsafa hiyo, amani, mshikamano na upendo vitaendelea kuimarika kwenye nchi yetu.

Aliyasema hayo juzi wakati anafungua jengo jipya la Kituo cha Polisi Wilaya ya Lushoto, ambapo jengo hilo linachukua nafasi ya jengo la zamani ambalo lilijengwa tangu Agosti 25, mwaka 1919 ikiwa ni Makau Makuu ya Jeshi la Polisi la Tanganyika la Wakoloni.

Masauni pia amewataka wananchi kushirikiana na Serikali ili kuweza kuendelea kuona nchi inakuwa salama, na kuweza kufanya shughuli zao kwa uhuru huku wakijihakikishia amani, usalama, umoja na ushirikiano.

“Tushirikiane na Serikali kuona nchi inaendelea kuwa salama. Na kwa maana hiyo niendelee kuwaombea viongozi wetu wakuu kwa kudumisha amani. Na niendelee kusisitiza, ni muhimu kuendelea kuziishi falsafa za Rais Dkt. Samia. Rais ndiyo Nembo ya Taifa hili. Rais ndiyo amepewa dhamana ya kuiongoza nchi hii. Sisi wasaidizi wake ndiyo tunatakiwa tupange mikakati mbalimbali ili kumsaidia.

Masauni alisema ni jambo la kihistoria kwa wananchi wa Lushoto kupata kituo hicho, kwani Jeshi la Polisi la Tanganyika chini ya Usimamizi wa Uingereza, lilianzia Wilaya ya Lushoto, na hapo ndiyo ilikuwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Tanganyika.

Hivyo, kwa Rais Dkt. Samia kutoa fedha sh. milioni 417 amewasaidia wananchi wa Lushoto kuweza kupata jengo jipya la Kituo cha Polisi Wilaya ya Lushoto, lakini hata wananchi wenyewe walikuwa na ari ya kupata kituo hicho, kwani wamechangia kwa kiasi kikubwa kukamilika ujenzi wake.

Masauni alisema, uzinduzi huo umefanyika ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Mpango wa Jeshi la Polisi wa kuboresha na kusogeza huduma za kipolisi karibu na wananchi. Mpango huo umeungwa mkono na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia, ambapo kupitia hotuba yake (Masauni) ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2024/2025 aliyoiwasilisha bungeni mwaka huu, alieleza juu ya azma ya Serikali ya kuendelea kuboresha miundombinu ya Jeshi la Polisi na vitendea kazi ili kulifanya kuwa la kisasa zaidi.

“Katika utekelezaji wa mradi huu, nimesikia katika taarifa ya Kamanda wa Polisi kuwa walipata ushirikiano mkubwa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli na wadau wengine. Hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine, kwa kuonesha mfano katika utekelezaji wa mpango huu wa Serikali wa kuendelea kuboresha miundombinu ya jeshi letu la polisi.

“Aidha, kwa namna ya kipekee niwapongeze wananchi wote, maafisa na askari, na viongozi wengine wa wilaya hii kwa michango na hamasa kubwa waliyoitoa kuwezesha ujenzi wa kituo hiki.

Mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya Jeshi la Polisi yakiwemo makazi ya kuishi askari pamoja na vituo vya polisi ni suala endelevu katika nchi yetu na ni moja ya mikakati muhimu kwa Taifa letu, hivyo wananchi pia wanawajibu wa kuunga mkono harakati za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya polisi. Kama ambavyo nimetangulia kusema kuanzia mwaka huu wa fedha Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi,” alisema Masauni.

Masauni alisema, aidha, kupitia Mpango wa Ujenzi wa Vituo vya Polisi katika Kata/Shehia zote nchini, Serikali itaendela kuunga jitihada za wananchi, hivyo ameendelea kuwasisitiza wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kupitia kata/shehia zao kuendelea na maandalizi ya kutafuta maeneo na kuanza hatua za awali za ujenzi wa vituo hivyo na Serikali itaendela na hatua za ukamilishaji.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi alisema ujenzi wa kituo hicho uliannza mwaka 2015, lakini ilipofika mwaka 2016 ujenzi wake ukiwa hatua ya linta ulisimama kutokana na sababu mbalimbali, lakini ilipofika mwaka 2022, Serikali ilitoa fedha sh. milioni 417 kwa ajili ya ukamilishaji.

Mchunguzi alisema katika fedha hizo, sh. milioni 250 zilitolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Maendeleo, na sh. milioni 167 zilitolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) kupitia Tuzo na tozo. Lakini ili kufanikisha ujenzi huo, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, na Halmashauri ya Bumbuli (Bumbuli DC) walifanikisha ujenzi huo.