April 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi kuchunguza madai ya mwanafunzi kutupa kichanga chooni

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa


Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linaendelea kufanya uchunguzi juu ya mwanafunzi wa kidato cha nne (18) wa shule ya sekondari Nkasi ambaye anadaiwa kujifingua mtoto na kisha kumtupia chooni.


Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija,amesema kuwa wiki iliyopita mwanafunzi huyo akiwa mjamzito bila ya mtu yeyote kufahamu inadaiwa alijifungua mtoto kisha kumtupa kwenye choo cha shimo na yeye kuelekea shuleni kuendelea na masomo.

Masija amesema kuwa watu walisikia sauti za mtoto huyo zikitoka ndani ya choo hicho na taarifa hizo ziliwafikia Polisi,ambao walifika eneo la tukio na kumuokoa mtoto huyo ambaye yupo hai hadi sasa.


Amesema kuwa baada ya uokozi huo, mtoto huyo alikimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu huku wakifanya uchunguzi wa aliyefanya kitendo hicho ndipo walipombaini mwanafunzi huyo.


Masija amedai kuwa binti huyo baada ya kuhojiwa alikiri kufanya tukio hilo,ambaye alidai kuwa alifanya hivyo bila ya kujitambua na hajui nini kilimfanya amtupe mtoto huyo chooni mara tu baada ya kujifungua .


Pia amesema kuwa kwa sasa mwanafunzi huyo amekabidhiwa mtoto wake kwa ajili ya kumnyonyesha,huku akieleza kuwa katika kuuliza kwa wataalamu wa afya wanadai kuwa huenda binti huyo alikumbwa na tatizo la afya ya akili wakati akijifungua .


“Kuna wakati mwanamke anapokuwa mjamzito ukumbwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo la afya ya akili na kuwa ndiyo maana wanalifanyia uchunguzi suala hilo na kama itabainika kuwa alifanya kitendo hicho kwa kukusudia hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani,”.